Ziara ya kusambaza Ilani kwa vyama vya siasa

Kwa siku ya pili, AZAKi nchini Tanzania, zikiongozwa na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili.Onesmo Olengurumwa, na timu iliyoandaa Ilani ya Uchaguzi ya AZAKi 2024-2029, wameendelea kufanya ziara ya kusambaza Ilani kwa vyama vya siasa kwa lengo la kuleta karibu masuala yaliyo ibuliwa na AZAKi zaidi ya 300 kutoka kwa wananchi na kuwekwa katika Ilani yao ya uchaguzi ya 2024-2029.

Katika ziara ya leo, wamefanikiwa kukutana na viongozi wa kisiasa wa NCCR MAGEUZI, akiwemo Bw.Imani Mshindani, Naibu Katibu Mkuu na timu yake ambao wote walipongeza kazi ya kipekee iliyofanywa na AZAKi katika Kutengeneza Ilani hii, wameweka bayana  yakuwa Ilani hii itatumika kama dira muhimu Wakati wa uandaaji wa Ilani yao ya Uchaguzi ya 2024/2025,

Pia waliweza kuuliza maswali kadhaa juu ya  hali ya sasa ya kidemokrasia na utawala wa kisheria, wakiangazia juu ya sheria na kanuni ngumu za uchaguzi pamoja na hali ya wananchi kupoteza imani ya ushiriki katika masuala ya uchaguzi.

Kwa wakati huu ambao tunaelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa, viongozi hao wamependekeza AZAKZi na Vyama vya Siasa kuendelea kuwa na mijadala endelevu itakayopelekea ufanisi wa Ilani hiyo.

Timu hiyo ilitembelea pia Chama cha Wananchi (CUF), ambapo ilikutana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya na viongozi wengine ambao wote walieleza kuridhishwa kwao baada ya kubaini yakuwa Ilani ya AZAKi imegusa  kwa kiasi kikubwa masuala ya utawala wa kisheria, utawala bora na demokrasia kwani huo ndio msingi wao mkuu katika kutatua changamoto za kijamii na hatimaye kutupeleka katika Tanzania tuitakayo.

Viongozi hao pia walibahatika kutembelea Chama cha Siasa cha Alliance For Democratic Change (ADC) na kukutana na Naibu Katibu Mkuu wa ADC Bara, Ndug. Innocent Gabriel Siriwa, Kamishna Mkuu, Ndg. Abdallah na viongozi wengine ambao kwa umoja wao waliridhishwa na kupongeza kazi ya AZAKi iliyofanywa kupitia Ilani hiyo ya uchaguzi na kuweka bayana yakua Ilani hiyo imeleta pamoja sauti za mamilioni ya Watanzania katika kutafuta suluhu ya kudumu ya masuala mbalimbali ambayo ni changamoto kitaifa na kupelekea kuwa na Maendeleo Endelevu na Jumuishi katika Taifa lenye misingi ya kisheria na haki Binadamu.

THRDC
8.10.2024