Tarehe 21 Juni 2025, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Mawakili Zanzibar (ZLS) waendesha mafunzo kwa zaidi ya mawakili 50. Lengo ni kuimarisha uelewa wa haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji miongoni mwa mawakili wa Zanzibar.
Mratibu wa THRDC Zanzibar, Suleiman Mujuni Baitani, alieleza kuwa elimu zaidi inahitajika ili jamii itambue na kulinda haki zake. Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisisitiza ushirikiano wa mawakili na jamii ili haki iwafikie wananchi wote.
Rais wa TLS, John Seha, na Rais wa ZLS, Joseph Magazi, walisisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu kwa mawakili katika utoaji wa huduma bora za kisheria. Nae Jaji Makaramba alionya juu ya matumizi ya mawakili bandia na kuhimiza wananchi kutumia mawakili waliothibitishwa kisheria. “Uwakili ni taaluma ya heshima na uwajibikaji. Kujifanya wakili bila sifa ni kosa la jinai,”
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha mfumo wa haki na kuwatumikia wananchi kwa weledi.