Leo tar 24 Juni, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) pamoja na wadau wengine wa sekta ya haki, asasi za kiraia na serikali walikutana chini ya mradi wa SCATZ kujadili masuala ya utawala wa sheria, haki za binadamu na uwajibikaji wa pamoja.
Mgeni rasmi katika Mkutano huu alikuwa Mhe. Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, aliyetoa wito wa kuimarisha haki, uwazi na ushirikiano, wageni wengine ni Wakurugenzi na wakuu kutoka idara mbali mbali za serikali na asasi za kiraia. Nayo THRDC kupitia viongozi wake – Suleiman Baitani na Onesmo Olengurumwa – walisisitiza umuhimu wa uratibu bora na msaada kwa watetezi wa haki.
Mshirika mwenza Jamila Juma kutoka ZAFELA alieleza mchango wa wanawake na msaada wa kisheria kwa makundi yaliyo hatarini, huku Jaji Salma Ali akitoa tafakari juu ya nafasi ya mahakama kulinda katiba na haki.
Tukio hili ni hatua muhimu katika kujenga mfumo wa haki unaojumuisha na kuzingatia ushirikiano wa sekta zote.