THRDC, EAHRI, TCRF, UDSoL NA LST ZINAFANYA MAFUNZO YA SIKU 2 KWA WATETEZI WA HAKI ZA WATOTO NCHINI TANZANIA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Taasisi ya Haki za Binadamu Afrika Mashariki (EAHRI), Shule ya Sheria chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSoL), Jukwaa la Haki za Watoto (TCRF) na Shule ya Sheria kwa Vitendo (LST) kwa pamoja zinafanya mafunzo kwa watetezi wa haki za watoto nchini Tanzania. Mafunzo hayo yanafanyikia katika ukumbi wa Maktaba ya Shule ya Sheria kwa vitendo leo Julai 31 na kesho Agosti 01, 2024.

Akieleza malengo ya mafunzo hayo Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kisheria na kiutendaji kazi watetezi wa haki za watoto nchini. Mhe. Mathias Mgimba Haule kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu amesema kwamba wizara inashughulikia masuala yote ya watoto na makundi maalumu ikiwemo masuala ya kisera na kisheria. Mratibu wa Kitaifa wa TCRF amesema kwamba TCRF ni shirika wanachama linalotetea haki za watoto hapa nchini. Mkurugenzi wa EAHRI Dkt. Francis Magare amesema kwamba EAHRI inajihusisha na masuala ya utafiti, ushauri wa masuala ya haki za watoto na binadamu. Dkt. Veronica Buchumi kutoka UDSoL amesema kwamba UDSoL ni mdau wa haki za watoto na hufundisha masomo ya haki za binadamu ikiwemo haki za watoto.
 
Akifungua Mafunzo hayo mgeni rasmi Professor Emeritus Chris Maina Peter amesema kwamba mafunzo haya ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo kuna matukio mengi ya watoto kupotea na wengine kutekwa. Pia mafunzo haya ni muhimu zaidi kwasababu watoto ni kundi ambalo lipo hatarini zaidi. Professor Maina amesisitiza zaidi kwamba katika kundi la watoto kuna watoto ambao pia wapo hatarini zaidi ya wenzao kwa mfano watoto ambao ni wakimbizi, watoto wenye ulemavu, watoto wanaokinzana na sheria, watoto walio katika hali ya vita na watoto ambao wameasiliwa.

Sababu kubwa ya watoto kuwa hatarini Professor Maina amesema kwamba ni kwasababu watoto hawawezi kusisitiza kuhusu haki zao na hivyo ni rahisi kubaguliwa au kukosa haki zao kwasababu ya umri wao. Haki za watoto huvunjwa au huathiriwa zaidi na watu wenye maslahi binafsi kwa watoto kwa mfano wazazi au walezi wanaotaka kuozesha watoto au watu wanaotaka kuoa watoto.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Mtoto wa mwaka 1989 umeeleza katika Ibara ya 4 kwamba Mtoto ni mtu yeyote ambaye hajafikisha umri wa miaka 18 isipokuwa kama nchi husika itaweka utaratibu mwingine kuhusu watoto. Hivyo Mkataba huu umetoa upenyo wa nchi kutafsiri mtoto kwa namna yake inavyoona inafaa. Mkataba huu umeridhiwa na nchi 192 kati ya nchi 193 za Umoja wa Mataifa. Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Mtoto wa mwaka 1990 umeeleza kuwa mtoto ni binadamu yeyote ambaye hajafikisha miaka 18.

Katika ngazi ya Kitaifa Professor Maina amesema kwamba kuna Sheria ya Mtoto ya Tanzania Bara na Sheria ya Mtoto ya Zanzibar ya Mwaka 2011. Hii ni kutokana na kwamba suala la mtoto sio suala la Muungano. Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaeleza katika kifungu cha 4(1) kwamba mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 na kifungu cha 4(2) kinazungumzia maslahi mapana ya Mtoto.

Propfessor Maina amesisitiza pia kwamba watoto wanao wajibu wa kuwaheshimu wazazi na watu wazima kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Mtoto wa mwaka 1990. Mkataba wa Afrika Juu ya Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981 unaeleza zaidi kwamba mtoto anao wajibu wa kuwaheshimu wazazi, watu wazima na kuwatunza wazazi wake wakizeeka.

Mafunzo hayo yanajumuisha watetezi wa haki za watoto 50 kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Dodoma, Tanga, Ruvuma na Mtwara.  

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
Julai 31, 2024
Dar es Salaam, Tanzania