MKUTANO WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI NA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA

Leo, tarehe 30 Juni 2023, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya mkutano wa kuwaleta pamoja mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuwapa elimu ya kikodi.
Pamoja na elimu hii, TRA imelenga kuskiliza na kutatua kwa pamoja changamoto za kikodi zinazoikabili sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali. Mkutano huu umehudhuriwa na zaidi wa wawakilishi 300 wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Mmoja wa mgeni maalumu katika mkutano huu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza.
Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa amewakaribisha wageni wa mkutano huu na kuwaambia TRA kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yana changamoto nyingi sana, hasa kupitia mfumo.

Bw. Edmund Kawamala, ambae ni meneja wa TRA kwa kanda ya Kinondoni, ameifurahia adhara kubwa ya mahudhurio kwenye mkutano huu. Bw. Kawamala amesema kuwa "Mikutano hii ni mizuri sana. Haki za mlipa kodi ni nyingi sana, ikiwemo haki ya kupewa tarifa na hata haki za kukataa kodi kama huielewi. Mlipa kodi ana wajibu pia, wajibu wa kujiandikisha ili kulipa kodi, pamoja na wajibu wa kutoa taarifa sahihi na kulipa kodi sahihi"
Meneja huyo alielezea kwa ufupi elimu ya mlipa kodi kisheria, juu ya changamoto kubwa ya faini inayoikabili mashirika hayo. Bw. Edmund amewapa ahueni mashirika hayo kwa kuwaambia, "Kuna kifungu cha ufutaji faini kupitia mfumo wa kidijitali, sheria inaruhusu na haina mlolongo mrefu."
Pamoja na hayo, Bw. Edmund amehakikisha utayari wa mamlaka hiyo ya kodi katika kuhudumia jamii, "Mkituhitaji siku zote msisite kutuita. Hata kama kuna gharama za ziada, sisi tupo tayari kuzilipa ili tuwafikie."
Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)