Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu -THRDC wenye wanachama zaidi ya 300 waandaa mafunzo kwa watetezi wa haki za binadamu ambao ni wanachama wake wapya kutoka kanda zake zote 11 nchini Tanzania.
Mafunzo haya yanafanyika kwa siku mbili mkoani dodoma kuanzia Tarehe 17 mpaka tarehe 18 Machi 2025 yakilenga kuwajengea uwezo wanachama hao katika masuala ya usalama, kanuni na taratibu za mtandao, namna bora ya kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na uzingatiaji wa sheria.
Katika kutoa salamu na ukaribisho, Mratibu wa kitaifa wa mtandao wa watetezi Tanzania wakili Onesmo Olengurumwa aliweza kuwapongeza wanachama hao wa THRDC kwa maamuzi na utayari wa kujiunga na mtandao kwani hii inaonyesha wazi kuwa kazi zinazofanywa na Mtandao huu zinaonekana na ni dhahiri kuwa zinaigusa jamii moja kwa moja.
THRDC imefanya kazi kubwa kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu wanatambulika nchini na kuweza kufanya kazi kwa karibu na serikali katika kulinda na kutetea haki za binadamu nchini.
Aliongeza kuwa kama mtandao, THRDC ina sera kanuni na taratibu zake kwa wanachama wake , hivyo ni mihimu kwa wanachama wote kuzifahamu kiundani, kuelewa sheria za nchi zinazosimamia Mashirika na kuzifuata (compliance)
Alisisitiza kuwa watetezi wa haki za binadamu wanapaswa kufanya utetezi kwa kuzingatia sheria na kanuni zote za nchi na kutumia namna bora ya kufanya utetezi bila kusahau njia njia na mbinu sahihi za kajilinda na changamoto za kiusalama zonazotokana na kazi zao za utetezi.
Katika ufunguzi wa Mafunzo haya, mgeni rasmi ambae ni Raisi wa chama cha wanasheria Tanzania wakili Boniface Mwambukusi alisisitiza kuwa kazi ya utetezi wa haki za binadamu sio kazi rahisi Bali ni kazi ya wito na kujitoa kwa moyo kwani watetezi wa haki za Binadamu ni sauti kwa wasio na sauti, ni macho kwa wasio na macho na ni nuru ya haki kweye giza la dhulma.
Alikazia kwa kusema kuwa suala la utetezi wa haki za binadamu sio kosa la jinai bali ni suala la kikatiba na la kimataifa kwani Tanzania imeridhia mikataba Mingi ya kimataifa ya haki za binadamu isipokuwa michache.
Alimaliza hotuba yake kwa kuishukuru THRDC kwani imekuwa msaada mkubwa kwake na imekuwa ikimsaidia na kumtetea mara nyingi kila alipokuwa anapitia changamoto katika harakati zake za utetezi wa haki na usimamizi wa sheria.
Wakili Mwambukusi alimaliza kwa kutoa wito kwa watetezi kutimiza wajibu wao na kusshirikiana na serikali katika kufanya ushawishi wenye tija (advocacy) kuanzia ngazi za chini za vijiji mpaka ngazi za juu za wafanya maamuzi bila kusahau kutetea haki za wanaume kama ilivyo kasi katika kutetea haki za wanawake, kwani kuwaacha wanaume nyuma katika utetezi kunapunguza kasi ya kufikia malengo ya haki na usawa hata katika jamiii.
Mtandao wa Watetezi wa Haki. Za Binadamu - THRDC
17 March 2025
