THRDC-ZANZIBAR YAENDELEZA USHIRIKIANO NA JESHI LA POLISI KUPITIA KIKAO CHA KIMKAKATI

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar (TANZANIA HUMAN RIGHTS DEFENDERS COALITION (THRDC)-Zanzibar) umefanya kikao cha kimkakati na Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar pamoja na Wakili wa Jeshi la Polisi, kwa lengo la kuendeleza mahusiano ya kazi na kuimarisha msingi wa pamoja wa kukuza Utawala wa Sheria na Haki za Binadamu visiwani Zanzibar.


Kikao hiki kilijikita katika kujadili njia za kuboresha ushirikiano kati ya asasi za kiraia na Jeshi la Polisi, huku pande zote zikisisitiza umuhimu wa kuwa na tafsiri zinazoshabihiana za sheria, pamoja na kuandaa mikakati ya pamoja inayolenga kulinda na kuendeleza haki za binadamu katika jamii.


Masuala muhimu yaliyojadiliwa katika kikao hicho yalihusisha kuendeleza majadiliano ya wazi na ya kitaasisi kuhusu changamoto na fursa katika utekelezaji wa sheria, kukuza uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa kila taasisi katika kulinda haki za binadamu, kuandaa programu za mafunzo ya pamoja kwa maafisa wa polisi na wanachama wa THRDC kuhusu haki za binadamu, sheria na maadili ya kazi, kujenga mfumo wa mawasiliano ya haraka kwa ajili ya kushughulikia matukio ya ukiukwaji wa haki kwa ufanisi zaidi, pamoja na kutengeneza mazingira ya kuaminiana yatakayowezesha ufuatiliaji wa pamoja wa utekelezaji wa haki na sheria kwa uwazi na uwajibikaji.


Kupitia kikao hiki, THRDC-Zanzibar na Jeshi la Polisi wamedhihirisha dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano wenye tija unaojengwa juu ya misingi ya heshima, mawasiliano ya wazi, na lengo la pamoja la kujenga jamii yenye haki, usawa, na amani.


#THRDCZanzibar

 #HakiZaBinadamu

 #UtawalaWaSheria

 #UshirikianoKatiYaCSONaPolisi

 #Zanzibar

 #TunaSimamiaHaki