Leo 13 Mei 2025 – Kamati ya Habari ya Zanzibar (Zanzibar Media Committee – ZAMECO) imekutana katika ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (World Press Freedom Day – WPFD). Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi, tarehe 17 Mei 2025, yakihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari visiwani Zanzibar. Miongoni mwa wadau wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na Tanzania Media Women Association (TAMWA – Zanzibar), Media Council of Tanzania (MCT – Zanzibar), THRDC – Zanzibar, pamoja na waandishi wa habari maarufu na wale wachanga katika tasnia ya uandishi wa habari.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni:
"Sheria Rafiki ya Habari ni Chachu ya Uchaguzi Ulio Huru, wa Haki na Unaofanywa kwa Misingi ya Uwazi."
Pia Kamati imejadiliana kwa kina juu ya mipango ya pamoja katika kufikia malengo ya siku hii muhimu kwa mafanikio makubwa. Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuandaa mijadala ya kitaaluma, kampeni za kuhamasisha umma kuhusu haki ya kupata taarifa, pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuwa na mazingira ya kisheria yanayowezesha uandishi huru, wenye kuwajibika na wenye kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
THRDC Zanzibar inaendelea kujenga mshikamano miongoni mwa wadau wa habari kwa kuhakikisha haki ya uhuru wa habari inalindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya jamii nzima.