ZIARA YA MRATIBU KITAIFA KWA SHIRIKA LA COSITA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetembelea shirika mwanachama la Community Support Initiative - Tanzania (COSITA). COSITA ni moja ya wanachama hai wa Mtandao, ni shirika kongwe  mkoani Manyara lililoanzishwa mnamo mwaka 2010.

COSITA inafanya kazi katika mikoa ya Manyara na Arusha katika wilaya ya Monduli. Kwa sasa, shirika lina miradi 5, ambapo miradi 3 inalenga haki za mtoto. Kwa mkoa wa Manyara, jamii nzima imewapokea shirika la COSITA katika kutetea haki za watoto. Pamoja na hayo, lengo kuu la COSITA ni kuboresha maisha ya wafugaji, wakulima wadogo, wakusanya matunda, na jamii yenye kipato kidogo kwa kuchangia katika fursa za kimaendeleo katika kutokomeza umaskini.

Mkurugenzi wa COSITA, Bw. Patrice Gwasma amesema THRDC ni mlezi bora kwa COSITA. Msaada wa kutengeneza Mpango Mkakati wa mwaka 2020 kutoka THRDC, umewawezesha COSITA kuwa na miradi hii ambayo wanayo kwa sasa. Pamoja na hilo, mafunzo ya usalama wa kidijitali umeweza kuhifadhi data za shirika katika sehemu salama zaidi.
COSITA imekiri kuwa na changamoto nyingi;
•⁠  ⁠Changamoto za kifedha. Miradi mingi kwa sasa inatekelezwa na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, hivyo kuwanyima mashirika ya kizawa kupata ufadhili.
•⁠  ⁠⁠Upungufu wa vitendea kazi imara na vya kisasa.
•⁠  ⁠⁠Ukosefu wa uwezo wa kulipa wafanyakazi, hasa wale waliojifunza kazi na kuiweza kikamilifu.
•⁠  ⁠⁠Ukomo wa Mpango Mkakati wa shirika ni mwaka huu, shirika halina fedha ya kuchkua mtaalamu kwa ajili ya kutengeneza Mpango Mkakati mwingine.

Bw. Onesmo Olengurumwa, Mratibu Kifaifa, amepongeza kazi kubwa ya COSITA mkoani hapo. Ameshauri shirika hilo kukusanya rasilimali kwa kuungana ma mashirika mengine (Joint Call). Hata Mtandao pia unajitahidi kutafuta mbinu na njia za kuweza kuwainua wanachama wake.

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
31 Oktoba 2024