UZINDUZI WA KAMATI YA UHAMASISHAJI WA RASILIMALI ZA NDANI

Leo, tarehe 10 Juni 2024, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unayofuraha kutangaza rasmi kamati yake iliyozinduliwa tarehe 6/6/2024 kwa ajilii ya kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za ndani zitakazo saidia Mashirika wadau wa Haki za binadamu hapa nchini Tanzania. Kamati hiyo inaundwa na wakurugenzi 27 wa taasisi (Wanachama wa THRDC) zinazotetea haki za binadamu kwa lengo la kuimarisha utetezi na ulinzi wa haki za binadamu nchini Tanzania.

Sote tunajua kuwa ufadhili wa ndani kwa ajili ya mipango ya utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania unakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na changamoto ya uelewa wa masuala ya utetezi wa haki za binadamu.

Hivyo dhumuni kuu la kamati hii ni kutoa mwongozo na kuunga mkono juhudi za mashirika ya utetezi wa haki za binadamu katika kukusanya rasilimali, pamoja na kutambua na kutekeleza mipango ya ubunifu ya kifedha kwa kuzingatia vyanzo vya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yao ya uendeshaji na uendelevu kifedha. Kamati hiyo imepewa majukumu mbalimbali, ikiwemo kutanua wigo wa ufadhili nchini Tanzania kwa kuandaa mkakati wa kitaifa wa kushawishi sekta binafsi kusaidia mashirika yote ya haki za binadamu hapa nchini yakiwemo mashirika wanachama na yasiyo wanachama wa THRDC.

THRDC inawakaribisha jamii ya sekta binafsi nchini Tanzania kuunga mkono hatua hii kwa sababu faida za kusaidia shughuli za haki za binadamu ni nyingi. Pia tunatoa wito kwa wanachama wa Mtandao na taasisi nyingine za haki za binadamu nchini Tanzania kuunga mkono mpango huu wa uendelevu wa kazi za haki za binadamu nchini Tanzania.

Bonyeza Hapa kupata dokomenti

Imetolewa na;
Wakili Onesmo Olengurumwa
Mratibu Kitaifa - THRDC