Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Vyama vya Wanasheria Wapanua Ushirikiano na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Uboreshaji wa Utoaji Haki Nchini

Dodoma, 17 Machi 2025 – Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Afrika (PALU), Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) wamefanya ziara na mazungumzo na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa lengo la kujadili fursa za kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya haki nchini. Walioshiriki katika ziara hii ni pamoja na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika - TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, Katibu wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki - EALS, Wakili John Seka, pamoja na wawakilishi wa taasisi shiriki wakiongozwa na Wakili Onesmo Olengurumwa - Mratibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu. Wajumbe hawa waliipongeza THBUB kwa juhudi zake za kulinda na kuendeleza haki za binadamu, hususan kupitia ushauri kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba ya haki za binadamu, pamoja na juhudi za kusukuma mbele utawala bora kwa kuzingatia misingi ya haki.

Wajumbe wa ziara hii walisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na THBUB katika maeneo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa serikali, taasisi za umma, na sekta binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora. Wajumbe walibainisha kuwa ushauri thabiti kwa serikali unaweza kusaidia kutengeneza sera na sheria zinazojibu changamoto za ukiukwaji wa haki, hususan katika kesi za unyanyasaji wa kijinsia, ucheleweshaji wa haki, na haki za makundi maalum kama watoto na watu wenye ulemavu. Pia, walisisitiza umuhimu wa kuhamasisha kuridhia na kutekeleza mikataba ya haki za binadamu kwa kuhakikisha kuwa Tanzania inatekeleza kikamilifu mikataba ya kikanda na kimataifa inayolinda haki za watu wake. Katika hilo, walipendekeza kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba hii, ili kuhakikisha kuwa haki zinadumishwa si tu katika sera, bali pia katika utekelezaji wake wa kila siku.

Katika hitimisho la kikao, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, na Katibu Mtendaji wa Tume, Kamishna wa Tume, waliisifu THRDC na vyama vya wanasheria kwa mchango wao mkubwa katika kukuza haki za binadamu, hususan kupitia upatanishi na usuluhishi wa migogoro inayohusiana na haki za binadamu, kusaidia watu waliokosa haki zao au walio hatarini kupata msaada wa kisheria, na kufanya tafiti zinazosaidia kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki za binadamu na utawala wa sheria. Waliahidi kuwa THBUB itaendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika, kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu haki zao, na serikali inapata mwongozo wa kitaalamu juu ya maboresho ya mfumo wa haki. Mazungumzo haya yanaashiria hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki nchini, ambapo ushirikiano kati ya THBUB na wadau wa haki za binadamu utasaidia kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa haraka, kwa usawa, na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Imetolewa na THRDC
 17 Machi 2025, Dodoma