Matembezi ya Amani ya Kulinda Ulinzi wa Watoto wa Tanzania

Leo September 14 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu - THRDC kwa Kushirikiana mashirika wanachama ambao ni watetezi haki za watoto  wameungana katika matembezi ya amani ya kudai ulinzi wa watoto wa Tanzania   Kwa kauli mbiu isemayo “Hakuna Ukimya tena  tunadai ulinzi wa watoto wetu “ kwani Tanzania bila ukatili kwa watoto inawezekana.

Huu ikiwa ni mwendelezo wa harakati ambazo THRDC  imekuwa ikizifanya  kwa kusapoti wanachama wake kutetea haki za watoto nchini ambapo Hatua hii ya matembezi ya amani imechukuliwa na wanachama hawa wa haki za watoto kama mojawapo wa njia  ya kuonyesha hali mbaya   Ya ukatili wa watoto iliyopo katika jamii yetu na kuonyesha kutokuridhishwa na matukio ambayo yamekuwa yakitokea hivi  karibuni kama mauaji, Ulawiti, Ubakaji, utekaji na hata utumikishwaji kwa kulinganisha na hatua za kisheria zinazochukuliwa  kuonekana kulegalega na kutoendana na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto wetu kila siku.

Takwimu zinaonesha Wazi ongezeko la ukatili kwa watoto  ambapo Ripoti za Takwimu za Msingi za mwaka 2023
zinaonyesha ongezeko la matukio ya ubakaji na ulawiti, ikiwa ulawiti  umeongezeka kutoka kesi 1,205 mwaka 2020 hadi 2,488 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 57. Pia Ubakaji umeongezeka  kwa kasi kutoka matukio 6,827 mwaka 2022 hadi 8,691 mwaka 2023, hii inadhihirisha tuko katika jamii isiyo salama kwa watoto

Hivyo  sisi kama Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu kwa kuungana  na mashirika wanachama wetu wa haki za watoto  kupitia matembezi haya tunalaani vikali vitendo vya kubakwa, kulawitiwa,
kutekwa, kupotea, kuibiwa na mauaji ya watoto vinavyoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwani Vitendo hivi ni kinyume na haki za binadamu ambazo Tanzania imeridhia kuzitekeleza katika mikataba ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo mkataba wa kimataifa
wa haki ya mtoto   Na mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa mtoto ambayo imetoa wajibu nchi kwa wanachama kuhakikisha inaweka mifumo itakayotoa ulinzi stahiki kwa mtoto bila ubaguzi na kuhakikisha watoto wanafurahia haki zao  kama zilivyoainishwa.

Pia wanachama hawa walitoa  wito na kuiomba serikali kuchukulia kwa uzito matembezi  haya  na matamko Mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu - THRDC na  wadau wengine kwani huku mtaani hali ni mbaya sana inaumiza na kukatisha tamaa.

Walisisitiza  haya kwa kumuomba Mheshimiwa Raisi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dr. Samia  Suluhu Hassan kutoa tamko  au kuchukua hatua akiwa kama mama  na kiongozi anaethamini  haki za watoto haswa haki ya ulinzi na haki ya kuishi ya kila Mtoto wa kitanzania.

Inetolewa na THRDC
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
September 14,2024
Dar es Salaam Tanzania