MAFUNZO KWA WATETEZI WANAOTOA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA KANDA YA PWANI MASHARIKI (Daresalaam, Pwani, na Tanga).

 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unashiriki katika utoaji wa elimu ya kisheria na haki za binadamu kwa watetezi wanaotoa huduma za msaada wa kisheria wa kanda ya pwani mashariki (inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga). Mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Afrika Mashariki (EAHRI), Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Daresalaam-Shule ya Sheria, na Shule ya Sheria ya Tanzania (LST).
Mafunzo haya ni ya siku mbili tarehe 7-8 Agosti 2023 na yanafanyikia katika Ukumbi wa Maktaba ya Shule ya Sheria ya Tanzania (LST). Kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Dkt. Clement Mashamba kutoka LST, Dkt. Veronica Buchumi kutoka Chuo Kikuu cha Daresalaam (Shule ya Sheria), Bw. Blastus Kahemela ambae ni wakili wa serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, na Bw. Onesmo Olengurumwa Mratibu Kitaifa kutoka THRDC
wameipongeza timu zima ya maandalizi na wahudhuriaji, kwa hatua hii ya kuwanoa watoa huduma za msaada wa kisheria. Kwa namna ya kipekee wamewakaribisha wanafunzi wa kozi hii fupi, na kuwahamasisha kutumia nafasi hii kuelimika zaidi katika masuala ya sheria na haki za binadamu.
Wakufunzi katika mafunzo hayo ni kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Haki za Binadamu ya Afrika Mashariki, Shule ya Sheria ya Tanzania, pamoja na Chuo Kiku cha Dar es Salaam - Shule ya Sheria.
Mafunzo haya ambayo yanawafikia watoa huduma 60, yanalenga kuwajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi watoa huduma hawa katika kazi zao za kila siku na hatimae kuwa na jamii yenye kuheshimu haki na usawa kwa watu wote.
Msaada wa Kisheria: kwa Haki, Usawa, Amani, na kwa Maendeleo
Imetolewa na;
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
7 Agosti 2023.