Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watetezi wanawake wa haki za binadamu

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unahudhuria maadhimisho ya siku ya watetezi wanawake wa haki za binadamu, leo tarehe 29 Novemba 2022. Maadhimisho haya yanafanyika jijini Dodoma, yakiratibiwa na Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (CWHRD).

Katika maadhimisho hayo, CWHRD imeahidi kuzindua ripoti ya awali ya hali ya wanawake watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania ambayo itatuonesha kitakwimu hali hiyo. Pia, CWHRD imedhihirisha mafanikio yake ya miaka mitatu ikiwa ni pamoja na kujengea uwezo watetezi, kutoa msaada wa kisheria, na utambulikaji wa kazi za wanawake watetezi wa haki za binadamu.

Siku hii ni siku ya kutambua, kuthamini, na kuonesha heshima ya kipekee kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu pamoja na watetezi wa haki za wanawake.

Muwakilishi wa THRDC, Bi. Lisa Kagaruki ameungana wa watetezi hao na kutoa rai kwa watetezi juu ya kuendelea kupambania nafasi ya watetezi. Katika kupambania nafasi hiyo, itambulike ya kwamba hadi sasa bado hakuna sheria yoyote Tanzania inayomtambua “Mtetezi wa Haki za Binadamu”. Hivyo tuendelee kutetea uwepo wa sheria hiyo.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali aliewakilishwa na Bw. Charles Mpaka. Wageni wengine ni pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya kamishna mkuu wa haki za binadamu(OHCHR), UN Women, WFT, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Freedom House, Wizara ya Katiba na Sheria.

Imetolewa na:
Afisa Habari
THRDC
29 Novemba 2022