Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, Onesmo Olengurumwa, akiambatana na Mratibu wa Kanda ya Pwani ya Kusini Bw. Clemence Mowmbeki pamoja na Afisa Dawati la Wanachama Bi. Lisa Kagaruki hii leo wametembelea shirika la Volunteer For Youth in Health and Development (VOYOHEDE) lililopo katika manispaa ya Mtwara.

VOYOHEDE ni Shirika la Utetezi wa Haki za Binadamu lililoanzishwa mwaka 2011 na linajihusisha na Utetezi katika pamoja na utoaji elimu katika maswala ya Afya na Uchumi na jinsia kwa makundi ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu, huku shirika likifanya kazi kuendana na malengo ya maendeleo endelevu namba 1, 3, 5, na 16.

Pia taasisi ya VOYOHEDE inajihusisha na utoaji wa msaada majumbani (HOME BASED CARE) na kuweza kuwapata na kuwafikia walengwa na kuwapatia misaada mbali mbali ya vyakula pamoja na elimu ya afya, taasisi inafika katika shule mbali mbali kutoa elimu ya Afya ya Uzazi (Reproductive Health), Maswala ya Amani na Haki (Peace and Justice) pamoja na utoaji wa elimu ya maswala ya ujasiriamali kwa vikundi mbali mbali.

Katika maswala ya uchechemuzi (Advocacy) VOYOHEDE imekuwa ikiwahusisha viongozi wa serikali katika hoja mbali mbali zinazoibuka katika utekelezaji wa miradi, ikiwemo usaidizi wa vifaa kama viti mwendo, kwa kundi la watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, taasisi imesaidia kuhamasisha kusogezwa karibu kwa huduma za upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI ambapo hapo awali wagonjwa walihitajika kusafiri umbaali mrefu na kutumia nauli kubwa uzifuata huduma hizo mijini.

Kwa mwaka 2021 pekee taasisi ya VOYOHEDE imefanikiwa kuwafikia wanufaika 169 kwa shuguli za moja kwa moja, watu 388 katika huduma ya utoaji wa msaada majumbani (HOME BASED CARE), na watu 262 wanaoishi na virusi vya UKIMWI wakifanikiwa kuhudumiwa kupitia vipindi vya redio vinavyoandaliwa na taasisi pamoja na makongamano mbali mbali.

Taasisi ya VOYOHEDE inakiri kunufaika na usaidizi wa THRDC katika uwezeshwaji wa kuandaa Mpango mkakati wa shirika ambao hapo kabla ungehitaji shirika kugharamia kiasi kikubwa cha pesa ili kuandaliwa.

“Tunaishukuru THRDC, kwa kutuwezesha katika uandaaji wa Mpango mkakati (Strategic Plan 2020/2024) ambao kwa kiasi kikubwa umetuwezesha kupata fedha za kuendesha mradi, kwa tayari taasisi ilikuwa imekaa miaka minne bila kuwa na mradi wowote” Deogratius Makoti, Mkurugenzi VOYOHEDE

Pamoja na mafanikio makubwa ya Shirika la VOYOHEDE, bado linakumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo, Kutokuwa na uwezo wa kutosha katika uandishi wa miradi ikiwemo miradi ya Haki za Binadamu, lakini pia taasisi haina uelewa mkubwa wa maeneo ambayo wafadhili wanazingatia katika utoaji wa fedha za miradi ya utetezi wa haki za binadamu, Ugumu wa kufikia maeneo ya mipakani (Karibu na Msumbiji) ambapo mara nyingi hukumbwa na vurugu za mara kwa mara.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Oktoba 17, 2021