ZIARA YA MRATIBU THRDC KUWATEMBELEA WANACHAMA WA THRDC INAENDELEA KANDA YA PWANI
 
Dar es Salaam, Tanzania
 
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa anaendelea na ziara ya kuwatembelea wanachama wa THRDC kwa lengo la kuendelea kufahamu kwa undani kazi zinazofanywa na watetezi hawa lakini pia kubaini baadhi ya fursa na changamoto wanazopitia katika kazi za utetezi. Ziara ya leo imeanzia katika taasisi ya Mtandao kwa Mashirika ya Haki za Binadamu yaliyopo Kusini mwa Afrika (SAHRiNGON).
 
Taasisi hii imeanza kufanya kazi tangu mwaka 1998 ikiwa moja ya wa wanachama wa mwanzo kujiunga na THRDC pamoja na wanachama wengine kama Morogoro Paralegals, TAWLA, LHRC, WILAC na SHRPC. Kwa sasa SAHRiNGON ina wanachama zaidi ya 100, huku 85 tu kati yao wakiwa ni wanachama hai.
 
Pamoja na SAHRiNGON kuwa na ushawishi mkubwa katika kupenyeza ajenda zake na kuwa na wanachama wengi, bado Mtandao huo unakumbana na changamoto kadha wa kadha za kiuendeshaji ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa fedha za kujiendesha.
 
Pamoja na changamoto hiyo ya kifedha pamoja na kuwa na wafanyakazi wachache, bado SAHRiNGON imekuwa ikiendeleza shughuli zake kwa kujitolea na kufanya mikutano ya menejimenti na bodi kama kawaida na ipo imara ikisonga mbele katika kazi ya utetezi.
 
Changamoto nyingine kubwa iliyopelekea kuyumba kwa taasisi hii ni pamoja na wakosoaji (Whistleblowers) ambao wamekuwa wakitoa taarifa za taasisi moja kwa moja kwa wafadhili.
 
“Mkosoaji ni mtu mzuri kwa shirika au taasisi yoyote ile lakini pindi akitumika vibaya, anaweza kuiharibu taasisi na kuipelekea kuyumba kabisa”, Martina Kabisama.
 
Mama Kabisama anazishauri taasisi kuhakikisha zinaweka nyaraka zake vizuri kwa ajili ya kumbukumbu za baadae kwani utunzaji wa nyaraka umeisaidia sana taasisi hiyo kuwa na nyaraka za zaidi ya miaka mitano.
 
Ameongeza kuwa, katika matumizi ya fedha za mfadhili ni vema kuzingatia matumizi sahihi (Cross Financing) kuepuka changamoto zisizo za lazima.
 
“Usitumie fedha ya mfadhili kwa jambo lingine tofauti na mlivyokubalina. Hii imeigharimu sana taasisi ya SAHRiNGON”, Martina Kabisama.
 
 
Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Tarehe 19 Machi, 2020