Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa ameanza rasmi ziara yake ya kutembelea wanachama wa kanda ya pwani ya kusini. Ziara hiyo imeanza na mkoa wa Lindi kwa mashirika wanachama mkoani humo.

Akiongozana na Mratibu wa kanda hiyo, Bw. Clemence Mwombeki, Mratibu Kitaifa pamoja na Afisa mkuu wa dawati la wanachama wameanza ziara katika shirika la Rondo Women’s Development Organization (ROWODO)

ROWODO ilianzishwa mnamo 2011 na kikundi 1 cha msingi ambacho kilishiriki sana katika kilimo kidogo na uhifadhi wa mazingira. Hadi sasa, shirika lina wanachama 10, watatu wakiwa wanachama wakiume.

Shirika limefanya kazi ya kuwezesha jamii juu ya elimu ya afya ya uzazi kwa vijana shuleni, uhifadhi wa mazingira, haki za binadamu na lishe.

Pamoja na Utoaji wa Elimu hizo, Shirika la ROWODO linasaidia vikundi vya kinamama katika usajili, kuunda uongozi pamoja na kusaidia upatikanaji wa vifaa kama viatu na kama vinavyowezesha vikundi vya kinamama kulimia zao la Mwani ambalo linalimwa sana katika mwambao wa bahari mkoani humu. Kwa mwaka 2021, ROWODO imeweza kuongeza vikundi 5 zaidi vilivyopo ngazi ya manispaa.

Katika eneo la uwajibikaji, ROWODO inafanya kazi kuhakikisha uongezekaji wa ushiriki wa wananchi katika kulinda na kusimamia miradi ya maji, kuongeza uwazi na uwajibika katika utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na kuhamasisha wadau wa maji kuzingatia sera na sheria za maji.
ROWODO limekuwa likishirikiana vizuri na mamlaka mbalimbali ikiwemo jeshi la polisi, uongozi wa mkoa, Mamlaka ya Maji (RUWASA) kwa nia ya kuhakikisha wananchi wanasaidika katika masuala yote ya haki ikowemo upatikanaji wa maji.

Pamoja na mafanikio makubwa ya shirika, ROWODO inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo;
• Uelewa mdogo katika uandishi wa miradi, jambo linalopelekea shirika kuwa na mianya michache ya upatikanaji fedha kwa ajili ya kuendeshea miradi
• Changamoto ya kifedha
• Changamoto ya wanachama kujitoa katika kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi mbali mbali ya shirika na kutarajia fedha kila wanapohitajika kushiriki.

ROWODO Inakiri kufurahishwa na fursa inazopokea kutoka katika Mtandao kama wanachama zinazowezesha taasisi kutambulika hadi ngazi ya kitaifa na kimataifa. Mfano kuonekana katika machapisho mbali mbali hasa chapisho la Nafasi ya AZAKI juu ya janga la UVIKO 19 lililochapishwa na THRDC.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
16 Oktoba, 2021