Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa Akiwa na Afisa Dawati la Wanachama THRDC Bi Lisa Kagaruki hii leo wametembelea taasisi ya Mchomoro Aids Combat Group (MACG – NGO) iliyopo wilayani Namtumbo, Mkoani Ruvuma.

Taasisi ya MACG- NGO imeanzishwa mwaka 2002 na inafanya kazi ya utetezi wa haki za binadamu katika maswala ya utoaji wa elimu ya afya na kuwatunza watu wanaoishi na maaambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kushawishi matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi kwa wagonjwa. Pia wanatoa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa sasa taasisi haina mradi wowote lakini imekuwa ikitumia mbinu ya kujitolea kufanya kazi mbalimbali kuisaidia jamii. MACG- NGO imekua ikishirikiana kwa ukaribu sana na halmashauri katika utoaji wa elimu mbalimbali kama njia moja wapo ya kuisaidia serikali kutimiza majukumu yake kwa jamii, na kulijenga taifa bora kwa ujumla.

Kutokana na taasisi Kutokuwa na mradi wowote uliofadhiliwa tangu kuanzishwa kwake, imejipanga kuanzisha mradi wa kilimo Cha mpunga. Hii ni kwasababu ya mpunga kuwa moja ya mazao yanayoiletea faida kubwa wilaya ya Namtumbo. Kilimo hichi kitaisaidia taasisi hii kujiendeleza kwa fedha zitakazopatikana kutoka kwenye mradi huo.

Mratibu kitaifa, Bw. Onesmo amewapongeza kwa hulka ya kujitolea ili kuhudumia jamii hata pale walipokosa kabisa wafadhili. Amewatia moyo kwamba waendelee kufanya kazi, jamii inawahitaji katika maeneo mengi sana ya haki za binadamu, hasa kwa kuangalia ya kwamba wilaya ya Namtumbo haina Asasi ya Kiraia nyingine inafanya kwenye eneo la haki za binadamu.

Pamoja na hayo, Bw. Olengurumwa aishauri MACG-NGOs kuisajili shirika hilo kama wasaidizi wa kisheria kwa wilaya ya Namtumbo ili waweze kuwafikia wengi sana na kufanya mengi zaidi kwenye jamii hiyo.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
19 Oktoba 2021