ZIARA YA MRATIBU KITAIFA WA THRDC NA AFISA DAWATI LA WANACHAMA YAANZA LEO KATIKA UKANDA WA PWANI

Dar es Salaam, Tanzania

Ziara ya Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Ndugu Onesmo Olengurumwa akiongozana na Mratibu Msaidizi wa THRDC Kanda ya Pwani Bw. Michael Marwa pamoja na Afisa wa Dawati la Wanachama THRDC Wakili Joyce Eliezer, imeendelea tena leo Mkoani Dar es Salaam. Ziara hii ni muendelezo wa ziara iliyokwishaanza mwezi wa pili mwaka huu katika ya tarehe 13 hadi tarehe 17 katika kanda ya Kaskazini Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na Kanda ya Pwani Mkoa wa Tanga na sasa hivi katika Mkoa wa Dar es Salaam uliopo katika Kanda ya Pwani. Shughuli kuu katika ziara hii ni kufanya mazungumzo na mashirika wanachama wa THRDC kuhusu fursa na changamoto katika kazi zao za utetezi wa haki za binadamu nchini na namna wanavyofanya kazi za utetezi wa haki za binadamu.

Mratibu Ndugu Olengurumwa na timu yake wameanza ziara yao leo kwa kulitembelea shirika la Mtandao wa Wanawake Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (Tanzania Network of Women Living with HIV – TNW+); ambalo ni shirika mwanachama wa mtandao (THRDC).

Akizungumza na Mratibu Kitaifa wa THRDC alipotembelea shirika hilo, Mkurugenzi wa TNW+, Bi. Joan Chamungu amesema, “Ni vema sasa asasi zingine za kirai nchini kulitambua pia kundi la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, kuwathaminia na kuwaweka katika ajenda muhimu za maswala ya haki za binadamu…Kundi hili la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali, hasa kunyanyapaliwa katika muktadha mbalimbali na kuonekana ni watu wasio na uwezo katika maswala yoyote yanayohusu maendeleo katika jamii.”

“Ukimjengea uwezo mwanamke anayeishi na virusi vya ukimwi, anaweza kufanya maendeleo makubwa katika jamii. Unyanyapaa kwa maeneo ya mijini umepungua kwa kiasi kutokana na elimu zinazotolewa katika vituo vya afya, familia na mashuleni. Kwa vijijini, bado ni changamoto sana kutokana na mila na desturi za baadhi ya makabila.”, aliongeza Bi. Joan Chamungu.

[envira-gallery id=”5994″]

Baada ya mkutano huo, Mkurugenzi wa TNW+ Bi. Joan Chamungu, aliwakabidhi  wageni wake zawadi za maboksi ya Kondomu kama ishara ya kuhamasisha matumizi ya kinga kuepusha maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwenye jamii.

 

Imetolewa leo tarehe 13 Machi 2020,
Na: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)