Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, Bw. Onesmo Olengurumwa, akiambatana na Mratibu wa Kanda ya Pwani ya Kusini Bw. Clemence Mwombeki, pamoja na Afisa Dawati la Wanachama, Bi. Lisa Kagaruki hii leo wametembelea
shirika la Foundation for Community Involvement (FCI TANZANIA) lililopo mkoani Mtwara.

FCI TANZANIA ni shirika lililosajiliwa mwaka 2019 na linalojihusisha na masuala ya haki za binadamu kwa makundi maalum pamoja na vijana (walio ndani na nje ya mashuleni). Vijana hawa hujengewa uwezo kwa njia mbalimbali ikiwemo uwezo wa kiuchumi na stadi za kazi.

Kwa mwaka 2021, FCI imekua ikifanya kazi na wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono (FSW) kwenye maeneo ya upatikanaji wa huduma za kiafya, elimu ya mabadiliko ya tabia, na kuwajengea mazingira wezeshi kiuchumi. FCI imefanikiwa kuwafikia FSW 222 hadi Septemba 2021, na kuunda na kusimamia vikundi 12 vya FSW na kuwajengea uwezo kiuchumi hata kufika ngazi ya kukopesheka. Hii ni mafanikio makubwa maana huwabadilisha na tabia moja kwa moja.

Kwa vijana waliopo mashuleni, FCI imeendelea kujenga elimu ya afya ya uzazi hasahasa hedhi salama. Julai 2021, FCI imefanikiwa kugawa paketi za taulo za kike 283 kwa shule tatu wilayani humo kama sehemu ya kuwashika mkono vijana wa kike.

Pia FCI ina vilabu katika shule tatu zilizopo wilayani Mtwara, kila kilabu kikiwa na wanafunzi 25. Wanafunzi hawa hujifunza stadi za kazi na elimu za maisha (mfano mambo ya heshima na maadili ya kiafrika). Haya hufanyika kwa uwezeshaji wa kujitolea.

Changamoto:
• Uandishi wa miradi ni changamoto kubwa kwa FCI. Mkurugenzi ameshuhudia kuandika miradi zaidi ya 10 bila mafanikio yoyote
• Changamoto za kifedha

FCI imeshuhudia kushirikiana kwa ukaribu na mamlaka husika katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia walieleza ya kwamba katika kujengea uwezo, FCI hutumia miongozo rasmi iliyowekwa na mamlaka husika kama vile miongozo kutoka wizara ya afya.

Bw. Onesmo Olengurumwa awapongeza kwa kujitolea kwa jamii inayowazunguka, hasa vijana maana vijana ni jamii inayotegemewa sana na taifa. Amewashauri waendelee kujituma, na kutimiza wajibu kisheria ili kuepuka adhabu, kuendelea kuweka takwimu sahihi maana haya yatawasaidia kuboresha ukuaji wa taasisi.
Mratibu Kitaifa amehakikisha ya kwamba, kuanzia mwakani Mtandao inaweza kuwa na mtu maaalum kwa ajili ya kusaidia wanachama wake juu ya uandishi wa miradi (proposal writings) na fund raising kwa ujumla kama ilivyokuwa kwa kusaidiwa kuandika mpango mkakati wa shirika (Strategic Plan).

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Oktoba 17, 2021