Mratibu Kitaifa wa THRDC, Bw. Onesmo Olengurumwa akiwa pamoja na Afisa Mkuu wa Dawati la wanachama hii leo wametembelea Shirika la Haki za Binadamu Nandangala (SHIHABINA).

SHIHABINA ni shirika linalojihusisha na masuala ya uelimishaji wananchi juu ya haki na sheria mbalimbali. Dhumuni lao kuu ni kuongeza uelewa wa wananchi katika eneo zima la haki na sheria kupitia shughuli zifuatazo;
• Uhamasishaji watambue haki zao
• Usuluhisho wa migogoro ya kifamilia
• Uhamasishaji wa masuala mtambuka
• Uchokoaji wa taarifa
• Ufuatiliaji wa masuala ya rushwa. N.k

Ustawi wa SHIHABINA unachangiwa na shirika hilo kufanya kazi kwa ukaribu sana na mamlaka husika hasahasa afisa maendeleo ya jamii pamoja na AZAKI nyingine nane zilizopo wilayani hapo.

Shirika hili linapata changamoto kadhaa ikiwemo changamoto za kifedha, upatikanaji wa usafiri, na hata utambulisho rasmi unaowatambulisha pindi wanapotimiza majukumu yao.

Pamoja na changamoto hizo, SHIHABINA imefanikiwa kuwafikia wananchi wasiopungua 100,000 katika elimu ya haki na sheria, pamoja na msaada na ushauri wa kisheria.

Tangu SHIHABINA iwe mwanachama wa Mtandao, imekiri kufaidika kwa kupokea mafunzo ya ulinzi na usalama kama mtetezi wa haki za binadamu ambayo yamemsaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yake. Pia Mtandao umewasaidia kupata taarifa muhimu za utetezi wa haki za binadamu kwa haraka zaidi.

Bw. Issa Chijuni ambae ni Mkurugenzi wa SHIHABINA ameshauri kuwa Mtandao uwe unawapatia vitini vya taarifa kwa maana si muda wote wanakua wanapatikana. Pia ameshauri Mtandao kuwawezesha waratibu wa kanda kifedha, ili waweze kuwafikia wanachama wote ndani ya kanda kwa urahisi zaidi ili waratibu watambue changamoto zinazowapata wanachama hao kwa ngazi ya kimkoa.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
16 Oktoba 2021.