Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa, akiambatana na Mratibu wa Kanda ya Pwani ya Kusini Bw. Clemence Mwombeki pamoja na Afisa Dawati la Wanachama Bi. Lisa Kagaruki hii leo wametembelea shirika la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA) lililopo katika manispaa ya Mtwara.

FAWOPA ni shirika mwanachama wa mtandao wa THRDC lililoanzishwa mwaka 2004, na linajihusisha na watoto katika masuala ya elimu, utatuzi wa kesi mbalimbali za ukatili zinazowakumba watoto ambapo shirika humtumia wakili wa shirika kusimamia kesi hizo ili kuwezesha upatikanaji haki.

“Familia nyingi katika mkoa wa Mtwara, watoto wanalelewa na mama au bibi yani upande wa familia ya kike na mra nyingi huo upande haumiliki mali, wala rasilimali zozote kiuchumi na huu hupelekea watoto wengi kuwa kwenye hatari ya kutokusoma, kwa kuwa wazazi wanashindwa kuwasaidia hivyo sisi kama shirika tunawatambua na kuwasaidia” Afisa kutoka FAWOPA.

Shirika limekuwa likishirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ambapo shirika huandika ripoti ya nusu mwaka ya hali ya haki za binadamu kwa mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi ambapo ripoti hiyo hutumika kutengenezwa kwa ripoti ya kitaifa ya hali ya haki za binadamu ambayo huandikwa kila baada ya miezi 6 na Tume, lakini pia FAWOPA hufanya uangalizi wa matukio yote ya uvunjifu wa haki za binadamu, na masuala yanayohusiana na haki za binadamu kwa ajili ya ripoti hiyo ya kitaifa.

Pamoja na kazi kubwa zinazofanywa na Taasisi ya FAWOPA, bado taasisi inakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo:
• Namna ya kufuata sheria mpya mbalimbali zinazoongoza AZAKI,
• Changamoto ya utayari wa serikali katika masuala ya uchechemuzi na haki za binadamu yanayofanywa na watetezi wa haki za binadamu ambapo serikali imekuwa ikihitaji mashirikiano zaidi na taasisi zinazotoa huduma Zaidi kwenye jamii na si uchechemuzi,
• mashirika kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili hupelekea baadhi ya miradi kuchelewa au kutokufanyika kabisa.

Hata hivyo shirika la FAWOPA limemwomba mratibu kuendelea kuyasaidia mashirika ya Haki za binadamu katika uwajibikaji wa kisheria (Compliance) kwa njia ya kuwajengea uelewa zaidi ili kuziwezesha AZAKI kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Mratibu THRDC ameahidi kuweka utaratibu wa kuongeza fursa za kujengea uwezo (Capacity Building) kwa shirika zaidi badala ya mtu mmoja, Ili kuwepo na watu mbali mbali katika wenye uelewa wa mambo mbali mbali ikiwemo uandishi wa miradi.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Oktoba 17, 2021