Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa akiongozana na Afisa Dawati la Wanachama, Bi. Lisa Kagaruki wametembelea shirika la Door of Hope to Women and Youth Tanzania (DHWYT) lililopo mkoani Mtwara

DHWYT ni shirika mwanachama ambae pia ni ofisi ya Mratibu wa Kanda ya Pwani ya Kusini. DHWYT ilianzishwa mwaka 2017 likiwa linajihusisha na maswala ya utetezi wa haki za binadamu hususani uwezeshaji na usaidizi wa wanawake na vijana. Katika utetezi wa haki za wanawake na vijana, taasisi hiyo inaangazia katika maeneo ya Elimu, Afya na Maji kwa kunatumia dhana ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji kwa jamii (SAM) katika kufuatilia matumizi sahihi ya pesa za umma inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo katika kuhakikisha wanakuza uwajibikaji kwa wananchi na watendaji. DHWYT pia inajihusisha na uangalizi na uwajibikaji wa mamlaka kwa kuangalia matumizi ya fedha za umma zinazotoka serikali kuu pamoja na halmashauri kuelekea katika maeneo ya msingi kama Elimu, Afya na Maji.

Katika eneo la uwajibikaji, pindi kunapobainika changamoto zozote, taasisi huweka usahihisho kwa kujenge uwezo wa kiuongozi kwenye eneo la mifumo ya utolewaji huduma ili kukidhi mahitaji ya jamii husika.

“Tuna Program ya kila mwaka kuhakikisha madiwani wanapata mafunzo ili waweze kutumia rasilimali vizuri, na kuweza kutimiza majukumu yao kwa niaba ya wananchi.” Bw. Clemence Mwombeki, Mkurugenzi DHWYT

Bw. Clemence anaongeza kuwa taasisi yake inaamini kuwa vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kufanikisha ajenda za kitaasisi hivyo huvitumia zaidi katika maswala ya uwajibikaji.

DHWYT inafanya pia programu ya Wanawake katika Uongozi na imeweza kufikia kata 10 kwa kushirikiana na SwissAid tangu mwaka 2020. Programu hiyo inalenga wanawake na vijana kushiriki katika maswala ya umma na uongozi, ambapo masuala ya uongozi, shitika limelenga maeneo makuu 3:
• Uongozi wa Kiuchumi
• Uongozi wa Kisiasa
• Uongozi wa Kijamii

Yote haya ni kuwawezesha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi kwa kugombea katika nafasi mbali mbali. Kupitia mradi huo DHWYT tayari imeweza kuwafikia wanufaika 1081 ambao wana vigezo vya kushiriki katika nafasi za uongozi. Wanufaika hawa watapimwa katika uchaguzi ujao wa 2025.

Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hii, bado inakabiliana na changamoto kadhaa ikiwemo;

1) Changamoto za kifedha, kwani kutokana na maswala ya UVIKO 19, fedha kuelekea katika miradi mingine zimekuwa zikitoka kwa kusuasua kutoka kwa wafadhili.

2) Taasisi kutokuwa na ofisi yenye nafasi kubwa ya kutosheleza wafanyakazi wote kwa shughuli za kitaasisi pamoja na kimtandao kama mwakilishi wa THRDC kanda ya pwani ya kusini.

DHWYT ikiwa kama ofisi ya uratibu wa kanda (zonal coordinating unit) imeeleza ya kwamba, wanachama wa kanda ya pwani ya kusini kuwa na mategemeo makubwa sana na Mratibu wa kanda. “Wanachama wanategemea mimi kua na majibu yote ya maswali yao, hasa masuala ya kujengewa uwezo”.

Mratibu wa kanda ameomba Mtandao kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya waratibu wa kanda kuwafikia wanachama wao mmoja mmoja, ili kuweza kusikiliza changamoto zinazowakabili, na kuzifkisha kwenye ngazi ya secretariat.

Mratibu Kitaifa wa Mtandao amepongeza shirika la DHWYT kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia wanachama wa kanda ya pwani ya kusini na kuahidi kuangalia namna ya kufanya kazi na shirika hilo ili kuwezesha upatikanaji wa ofisi yenye nafasi kubwa itakayoweza kuhudumia jamii pamoja na wanachama wa mtandao kwa shughuli mbali mbali za kikanda. Mratibu Kitaifa aliongezea kuwa tayari Mtandao umeshapanga kuwa na vikao vya kikanda kwa wanachama wa Mtandao, ili kuongeza uimara wa Mtandao kwa kanda zote pamoja na kuwezesha utatuzi wa changamoto za wanachama kwa wakati.
Afisa dawati ameendelea kumuhimiza mratibu wa kanda kuwa karibu na wanachama wa kanda yake, na kuwahamasisha wawe wanachama hai wa Mtandao ili wasipitwe na fursa zilizopo.

Mratibu Kitaifa, Mratibu kanda ya pwani ya kusini, Afisa dawati la wanachama pamoja na afisa habari walitembelea pia ofisi inayotarajiwa kuwa ofisi DHWYT pamoja na THRDC kanda ya pwani ya kusini itakayokuwa inaratibu kazi za Watetezi kanda hii ya Pwani ya kusini.

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
17 Oktoba 2021