Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini Tanzania THRDC Onesmo Olengurumwa Akiwa na Afisa Dawati la Wanachama THRDC Bi. Lisa Kagaruki hii Leo wametembelea taasisi ya Tunduru Paralegal Center (TUPACE).

TUPACE ni kituo cha msaada wa kisheria wilayani Tunduru kinachojihusisha na utoaji wa msaada wa kisheria katika maeneo mbali mbali ikiwemo maswala ya Ndoa, Usimamizi Mirathi, Kesi za Ukatili wa kijinsi, Kesi za madai, masuala ya Ardhi, Matunzo ya watoto, pamoja na masuala ya Ajira. TUPACE imekuwa ikifanya kazi katika kata 39 za wilaya ya Tunduru zenye vijiji zaidi ya 134. Taasisi Ina wanachama ( Paralegals) 19 wanaoisaidia taasisi katika utekelezaji wa kazi hizo.

Taasisi ya TUPACE ina mafanikio mengi sana ikiwemo;

a) Kufahamika vyema kwa Jamii na Wadau wa maendeleo pamoja na kukua ambapo toka kuanzishwa kwake taasisi imejengeka na Kuwa na uwezo wa kufanya kazi za kuhudumia jamii kwa mujibu wa Katiba ya Shirika.

b)TUPACE imefanikiwa kuendesha program za utoaji elimu kwa jamii na huduma za msaada wa sheria kwa mtu mmoja mmoja kupitia wanachama wake (Legal Aid Providers) katika masuala ya Elimu ya Sheria pamoja na elimu kupitia vipindi vya radio na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

c) Utoaji wa elimu ya sheria katika makundi mbalimbali ambapo TUPACE imebuni njia nyingine mpya ya kuifikia jamii kwa karibu zaidi na kwa idadi kubwa ya wananachi wanaofikiwa kwa mfumo wa Elimu Mkoba (Outreach Program for Legal Education) ambapo team ya TUPACE imekuwa ikitembelea na kutoa elimu katika kata zote ambazo hazina paralegals wanaotoa elimu hiyo kwa mada za Elimu ya Sheria ya Mtoto 2009 na Athari za Ukatili wa Kijinsia katika shule ambazo imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi mashuleni.

d) Ushirikiano mkubwa baina ya TUPACE na Serikali pamoja na mashirika yanayofanya shughuli zinazofanana na TUPACE wakiwemo Mahakama,
Mawakili/Wanasheria na mitandao mbali mbali ya utetezi wa Haki za Binadamu.

Pamoja na mafanikio hayo TUPACE inakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo..

a) Ufinyu wa Bajeti za kuendeshea Miradi

b) Upungufu wa Paralegals (wasaidizi wa kisheria) katika Taasisi kutokana na Paralegals wengi kuacha kufanyakazi ya kujitolea au kuwepo kwa malipo duni.

c) Ukubwa wa eneo la kazi ukilinganisha na idadi ya wasaidizi wa kisheria waliopo ambao ni 19 tu kwa kata 39 zilizopo wilayani Tunduru. Hivyo kutokuwepo kwa uwiano na kupelekea msaidizi wa kisheria mmoja kufanya kazi kwenye kata zaidi ya 2 kwa mwezi ambao ni sawa na vijiji visivyopungua vitano hadi sita (5-6).

d) Ufinyu wa Bajeti na Usafiri wa kufikia vijiji na kata zikiwemo kata ambazo hazina watoa huduma za msaada wa sheria imekuwa kikwazo cha kuwafikia wananchi wenye uhitaji/changamoto za masuala ya upatikanaji wa haki.

f) Shirika kukosa wataalamu wa kutosha wenye weledi wa kutosha kuandika miradi kupitia miradi inayoitishwa na wafadhili.

Taasisi ya TUPACE imeazimia na kupendekeza yafuatayo katika utatuzi wa changamoto kadhaa zinazoikabili taasisi;

1. Uongozi wa TUPACE unaendelea kutafuta fursa za kupata fedha kwa kushirikiana na mitandao na wahisani mbali mbali ili kuhakikisha shirika linajikwamua na changamoto za kifedha zilizopo, ikiwemo kuwashauri kusaidia kuendesha mfumo wa utunishaji mfuko (Local Resources Mobilization)

2. TUPACE inatoa wito kwa maendeleo yakiwemo mashirika
kuisaidia taasisi katika upatikanaji wa fedha na vifaa vya kufanyia kazi kama kompyuta, magari nk, ili kwa pamoja taasisi iweze kuifikia jamii na kufanya Kazi kwa ufanisi zaidi.

Hata hivyo Mratibu Kitaifa THRDC ameipongeza taasisi ya TUPACE kwa kufanya Kazi kwa weledi na kuweza kufikia maeneo mbali mbali ya wilaya kwa msaada mbalimbali.

“Niwapongeze sana kwa Kazi nzuri, na bahati nzuri nimepata nafasi ya kuzungumza na mkuu wa Wilaya hii ya Tunduru DC. Julius Mtatiro amewasifu sana na kueleza namna mmekuwa mkiisaidia Serikali katika kutatua changamoto mbali mbali za kisheria zinazowakumba wakazi wa Tunduru, na ameahidi kuiendeleza ushirikiano na Taasisi ya TUPACE kwa maendeleo ya wana Tunduru” Onesmo Olengurumwa, Mratibu THRDC

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
19 Oktoba, 2021