Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini Tanzania THRDC Onesmo Olengurumwa akiambatana na Mratibu wa kanda ya Pwani ya Kusini Bw. Clemence Mwombeki, Pamoja na Afisa dawati la Wanachama Bi. Lisa Kagaruki wametembelea Shirika la Sports Development Aid Lililopo mkoani Lindi.

Shirika la Sports Development Aid ambalo lipo katika mikoa mitatu ya Tanzania Bara ( Lindi, Mtwara na Singida) limekuwa likiendesha miradi mbali mbali ikiwemo uhamasishaji wa Maswala ya usawa wa kijinsia, Haki za Binadamu, Pamoja na utunzaji wa mazingira kupitia michezo mashuleni.

Shirika limefanikiwa kusaidia idadi kubwa na wanafunzi kuondokana na utoro mashuleni, kumaliza shule, kuhamasisha mahudhurio, na hii imefanikiwa Kutokana na michezo ambayo imekuwa ikiendeshwa mashuleni kupitia taasisi ya Sports Development Aid.

Hata hivyo taasisi imekuwa ikiwatambua watoto wenye vipaji ambao wanatoka katika familia duni kuweza kuwasaidia kwa vifaa vya shule, kujiunga na Vyuo mbali mbali vya michezo na kuwezeshwa kujiendeleza kimaisha kupitia michezo na Mafunzo ya VETA Baada ya Elimu.

“Wapo watoto waliotambuliwa Kutokana na miradi yetu ambayo imefanikisha kupata watoto waliochaguliwa kujiunga na Club ya Yanga B, Pamoja na shule ya Alliance iliyopo mkoani Mwanza huku wengine wakipata ufadhili wa kusoma Nje ya nchi Ili kujiendeleza na vipaji vyao katika michezo” Ramson Lucas Meneja Mradi, Sports Development Aid.

Pamoja na Kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya Sports Development Aid Bado inakumbana na changamoto zifuatazo;

1) Changamoto za kisiasa zinaelezwa kuingilia baadhi ya miradi taasisi ambayo kwa kiasi kikubwa ililenga kuwaandaa waalimu katika Vyuo mbalimbali Kuwa na uelewa na Ari ya kupenda michezo Ili kuweza kuihamasisha mashuleni, japo Mpango huo ulisitishwa na kuacha Vyuo vichache vikiendelea na utaratibu huo na kupelekea kuwepo kwa walimu wachache wenye mapenzi na michezo na wanaoweza kuhamasisha michezo kwa watoto.

2) Changamoto za vipaombele kutoka kwa Serikali ambavyo vimepelekea baadhi ya miradi kuchelewa kutekelezwa kwa wakati.

3) Changamoto ingine ni ‘Sustainability’ pindi miradi Inapoisha na shule au Serikali kushindwa kuiendeleza miradi hiyo kwa mashule, lakini pia kuwepo kwa viwanja vichache vya michezo mashuleni kumepelekea watoto kushindwa kujihusisha na michezo.

Mratibu THRDC ameipongeza taasisi hiyo Kutokana na Kazi nzuri inayoifanya katika kuhamasisha michezo mashuleni utamaduni ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa umeanza kuachwa na kuishauri kuona uwezekano wa kuwa na Academy itakayowawezesha watoto kujiendeleza katika michezo mbali mbali ambayo kwa sasa imesahaulika kwa kiasi kikubwa.

Imetolewa na

Mtandao wa Watetezi wa Haki Binadamu
16 Oktoba, 2021