JAJI Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema masuala ya haki za Binaadamu ni kati ya vitu vya msingi sana kwa vile yanagusia stahiki ambazo zinampaswa kila binaadamu kuzifaidi.

Ameyasema hayo leo tarehe 19 Agosti 2021 wakati akifungua warsha ya siku mbili ya mawakili na wanasheria Zanzibar ambayo imeandaliwa na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) inayofanyika katika hotel ya Golden mjini Unguja.

Amesema kuwanyima watu haki zao, ni sawa na kuukanusha ubinaadamu wao na hakuna haki zenye uzito ambazo binaadamu anapaswa kuwa nazo,

Jaji mkuu huyo amesema matumaini i yake mkusanyiko huu pamoja na mambo mengine utajadili namna ambavyo mawakili wanapaswa kuendesha kesi zenye maslaqhi kwa umma, haki za binaadamu, uhuru wa kujieleza kwa viwango vya kitaifa na vile vya kimataifa.

Amesema katika mafunzo hayo mawakili hao watajifunza ufunguzi wa mashauri ya kimkakati na mambo mengine yenye mnasaba na utekelezaji wa haki za binaadamu.

Aliwaomba washiriki hao kuwa makini katika mafunzo hayo kwa vile, masuala yaliyopangwa kujadiliwa yanagusa msingi na heshima ya ubinaadamu.

“ Haki za Binaadamu ni kati ya vitu vya msingi sana kwa vile yanagusia stahiki ambazo zinampaswa kila binaadamu kuzifaidi kwa kuwa yeye ni binaadamu. Haki hizi kwa lugha nyengine huitwa ni haki ambazo binaadamu kuzaliwa nazo”alisema.Makungu

Naye Mratibu Kitaifa wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa, amesema mawakili hao watapata uzoefu na kuwasaidia wananchi wanapohitaji kusaidiwa kuendesha mashauri ya haki za kibinadamu na kikatiba.

Amesema wananchi wanapaswa kutumia njia za busara kudai haki kwa kwenda mahakamani na sio kwenda barabarani kufanya vurugu hivyo wakipata mawakili wa kuwasaidia watadai haki zao mahakamani.

“Mawakili na wananchi wakielewa vizuri kudai haki zao kupitia mahakama kutapunguza malalamiko na uonevua”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud, amesema mafunzo hayo ni ya kipekee ambayo yatawasaidia mawakili hao kutetea haki za binadamu.

Amesema kuwa kwa muda mrefu kuna utetezi lakini mawakili wanafanya kazi zao bila ya kuwa na mifumo na mipango mikakati ya kutetea wanapokua Mahakamani.

“Mafunzo haya yataongeza uwelewa na watakaposimama mahakamani wawe wanafanya utetezi kwa kujiamini na kufuata misingi na taratibu za sheria”alisema.

Alisema hivi sasa kuna mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hata watenda makosa wanambinu nyingi hivyo bila kuwa na mafunzo ya mara kwa mara kunasaidia kutuweka pamoja na kujua mbinu za watendaji makosa”alisema Jamila.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewashirikisha mawakili wa Unguja na Pemba na yameandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania nchini ya ufadhili wa American Bar Association (ABA).

Imetolewa

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu THRDC

19 Agosti 2021