WAANDISHI WA HABARI WATATU NA MMILIKI WA NJOMBE YETU TV WASHTAKIWA MAHAKAMANI NJOMBE

Njombe – Tanzania

Waandishi wa habari watatu wanaomiliki TV za Mtandaoni pamoja na mmiliki wa Njombe Yetu TV leo Machi 4, 2020 wameshtakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Waandishi hao ni: Prosper Daudi Mfugale mwandishi wa ITV ambaye anamiliki Njombe TV, Ibrahim Godfrey Mlele mwandishi wa TV-E anayemiliki Mlele TV, Dickson Kanyika mwandishi wa Star TV anayemiliki Habari Digital TV, pamoja na Benedict Kisawa ambaye ni mmiliki wa Njombe Yetu TV.

Kuhusu Kukamatwa Kwao:
Waandishi hao walikamatwa siku ya Jumamosi tarehe 29 Februari 2020 majira ya saa kumi jioni. Waandishi Prosper Daudi Mfugale, Ibrahim Godfrey Mlele na Benedict Kisawa walikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumiliki TV za Mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA). Pia, mwandishi Dickson Kanyika alikamatwa akiwa Morogoro mjini na kusafirishwa hadi kituo cha polisi Njombe mjini.

Kuhusu Mashtaka Dhidi yao:
Leo Machi 4, 2020 waandishi hao watatu pamoja na mmiliki wa Njombe TV walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na kila mmoja kusomewa shitaka lake na kupangiwa Hakimu wake atakayesikiliza kesi yake. Waandishi hao wameshtakiwa kwa kosa linalofanana la KUTOA HABARI MTANDAONI bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kinyume na kifungu namba 130(1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta sura ya 306 [Toleo la Mwaka 2017] pamoja na Kanuni ya 14(1) na 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) za mwaka 2018.

Wito wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC):
Mtandao unatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari mtandaoni, watumiaji wa mtandaoni, watunga sheria na wadau wote wa haki nchini kuendelea kupinga kanuni hizi ambazo kimsingi zipo kinyume na misingi ya haki ya uhuru wa watu kujieleza kwa kutumia njia yoyote ile ambayo wao wameichagua ikiwemo kutumia mitandao. Ikumbukwe kuwa mitandao ya kijamii ipo bure kwa kila mtu duniani kutumia na wenye mitandao hii hawajawahi kudai wanaotumia walipie chochote.

Ikumbukwe kwamba, mnamo mwezi Juni 2018 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), tulifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kanuni za Maudhui ya Mtandaoni kwa sababu, kwa kiwango kikubwa zinaminya uhuru wa watu kujieleza kinyume na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

 

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Machi 4, 2020