“UVUMILIVU, UMOJA NA KUBAKI KWENYE AJENDA YA SHIRIKA NI NGUZO YA MAFANIKIO YA SHIRIKA”

Uvumilivu, Umoja miongoni mwa Watetezi wa Haki za Binadamu pamoja na kubaki kwenye ajenda ya Shirika ni miongoni mwa nguzo muhimu katika Utetezi wa Haki za Binadamu nchini.

Haya yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki Madini Ndugu Amani Mhinda wakati wa ziara ya Mratibu wa THRDC Bw. Onesmo Olengurumwa.

Amani ametolea mfano jinsi ambavyo Shirika lao lilivyoyumba kifedha kutokana na Wafadhili wao kuhamia kwenye shughuli za Mafuta na Gesi. “Kama sio kuwa na msimamo wa kubaki kwenye ajenda yetu ya kutetea masuala ya madini tungejikuta tunahamisha ajenda zetu na kuhamia kwenye shughuli za mafuta na gesi ili kuweza kupata fedha”, amesema Mkurugenzi wa HakiMadini Ndugu Mhinda.

Pia Ndugu Mhinda amesisitiza umuhimu wa Mashirika Wanachama wa THRDC katika kila kanda kufanya kazi pamoja kama nguzo muhimu katika kufanikisha shughuli za Utetezi wa Haki za Binadamu nchini.