THRDC YAWAFUNDA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU UMUHIMU WA USAWA WA KIJINSIA NA USHIRIKISHWAJI WA MAKUNDI YA KIJINSIA KWENYE MAENDELEO YA JAMII:

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unaendesha mafunzo ya siku mbili (tarehe 12 hadi 13 Desemba 2019) kuhusu masuala ya haki na usawa wa kijinsia kwa wawakilishi 60 wa mashirika wanachama wa THRDC. Mafunzo haya yanafanyika katika ukumbi wa Kisenga, jengo la LAPF Tower mkabala na kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mafunzo haya yameandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuadhimisha kilele cha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia duniani; zilizoanza mnamo tarehe 25 Novemba 2019 na kufikia tamati juzi tarehe 10 Desemba 2019 ambayo pia ni Siku ya Haki za Binadamu Ulimwenguni.

Mafunzo haya ya siku mbili yanalenga kuoanisha haki za kijinsia na mchango wake katika kazi za utetezi wa haki za binadamu nchini.

Mafunzo haya yanayotolewa na THRDC yatakuwa chachu ya kuhimiza usawa wa kijinsia nchini hususani kwenye sekta ya Asasi za Kiraia, kama ambavyo imekuwa ikipigiwa upatu na Serikali pamoja na wadau wa haki za usawa wa kijinsia.

Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto ya mwaka 2000 iliyofanyiwa mapitio na kuwa Sera ya Jinsia mwaka 2005, imetambua mchango wa Asasi za Kiraia kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko muhimu ikiwemo kuleta usawa wa kijinsia pamoja na kukomesha ubaguzi. Hivyo THRDC kupitia mafunzo haya itaweka bayana umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia katika upangaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wanachama wake na Asasi za Kiraia kwa ujumla katika kuihudumia jamii ya watanzania.

Ikumbukwe pia, Usawa wa Kijinsia ni mojawapo ya Malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na ukosefu wa usawa wa kijinsia hupimwa kila mwaka na Umoja wa Mataifa kupitia ripoti za Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.