Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ,leo Januari 19,2022, unayo furaha kutembelewa na mwanachama wake, Mkurugenzi wa shirika la Tanzania Epilepsy Organization (TEO) Bi.Fides Uiso.


Katika Ugeni huo Bi. Fides Uiso ameeleza kazi zinazofanywa na taasisi ya Tanzania Epilepsy Organization ambayo imekuwa ikisimamia kituo chenye jumla ya watoto 25 wa kutwa na Bweni, ambao ni wahanga wa ugonjwa wa kifafa. Kituo hicho kinatoa huduma mbali mbali kwa watoto hao wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo mbali mbali ya kazi za mikono, mazoezi ya viungo pamoja na ushauri wa kisaikolojia kwa watoto na wazazi wa watoto wanaugua kifafa.

Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa amempongeza Bi. Fides kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatunza watoto na vijana hao wahanga wa kifafa pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuweza kufahamu zaidi juu ya ugonjwa huu.

Katika mazungumzo hayo, Mratibu THRDC, amemshauri Bi fides kuendelea kufungua milango ya mashirikiano na wadau,taasisi mbali mbali pamoja na wizara husika kwa ajili ya kuhakikisha wahanga wa ugonjwa wa vifafa wanapata huduma stahiki katika afya na maeneo mengine.

Kwa muda sasa THRDC imekuwa ikishirikiana na wanachama wake, pamoja na wadau mbali mbali wa haki za binadamu, kuhakikisha inashiriki katika kampeni na shughuli mbali mbali za kijamii kwa lengo la kurudisha tabasamu kwa jamii na makundi mbali mbali yenye uhitaji.

Pichani ni Mratibu wa kitaifa wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu akipokea Zawadi ya Kikombe kutoka kwa Bi. Fides Peter Uiso Mkurugenzi wa shirika la Tanzania Epilepsy Organization.