THRDC YASHIRIKI KONGAMANO LA HARAKATI ZA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA VISIWANI ZANZIBAR

THRDC YASHIRIKI KONGAMANO LA HARAKATI ZA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA VISIWANI ZANZIBAR

Zanzibar, Tanzania

Leo tarehe 28 Julai 2021, Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa ameshiriki Kongamano la Kutokomeza vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) ambalo pia ni shirika mwanachama wa THRDC. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil visiwani Zanzibar, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kongamano hilo liliwaleta pamoja viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwemo Jaji mkuu wa Mahakama ya Zanzibar, Makamishna wa Polisi, Mkurugenzi mkuu wa Mashtaka Zanzibar, Mrajisi wa Mahakama ya Zanzibar, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, pamoja na Wakurugenzi wa Asasi mbali za Kiraia kutoka mashirika ya FCS, LSF, KAS na THRDC.

Dhumuni kuu la kongamano hilo leo lilikuwa kuzungumzia changamoto ya ongezeko la matukio ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto visiwani Zanzibar licha ya kuwepo kwa Tume ya Kuratibu Mapambano Dhidi ya Udhalilishaji wa Kijinsia visiwani humo hususani matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto pamoja na talaka nyingi zinazochochea utelekezwaji wa wanawake wengi wanaoelemewa na majukumu ya kuwalea watoto peke yao.

Kwa mujibu wa taarifa ya tathmini ya mwenendo wa matukio ya udhalilishaji wa kijinsia iliyotolewa leo na ZAFELA, hadi kufikia mwezi Juni 2021, tayari kuna ongezeko la matukio takribani mia tano (500) ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yaliyokwisharipotiwa na wanajamii katika kipindi cha miezi sita (6) pekee. Hata hivyo, swali lililoibuka ni: “Je, ongezeko hilo ni ishara ya uelewa na mwamko wa wanajamii kuripoti matukio ya udhalilishaji wa kijinsia? Ama la!, ni ishara ya tatizo kuzidi kuwa kubwa ndani ya jamii?”.

Naye Mratibu Kitaifa wa THRDC Wakili Olengurumwa akiwasilisha salamu za wanachama wa THRDC kwa Mgeni Rasmi Rasi Mwinyi, amepongeza muendelezo wa mashirikiano mema kati ya Watetezi wa Haki za Binadamu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya jamii na kuiomba serikali na wadau wa maendeleo kuja pamoja katika kutafuta suluhu ya uhakika ya kutatua changamoto hii ya ongezeko la matukio ya udhalilishaji wa kijinsia visiwani Zanzibar ili kuimarisha haki za wanawake na watoto.

Kwa taarifa zaidi tafadhali bonyeza hapa kuangalia tukio zima la Kongamano la Harakati za Kutokomeza Vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar.

Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

Tarehe 28 Julai 2021