THRDC YAPATA RUZUKU KUBORESHA USHIRIKIANO KATI YA AZAKi NA MAMLAKA ZA NCHI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO

Shirika la kimataifa la PROTECTION INTERNATIONAL lenye makao yake makuu jijini Brussels nchini Ubelgiji na ofisi yake ndogo ya kanda jijini Nairobi, Kenya, limetoa kiasi cha Euro 256,539/-, sawa na Shilingi za Kitanzania Milioni 650 kama ruzuku kwa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Fedha hizo zinalenga kutekeleza mradi wa miezi 12 wa kuboresha ushirikiano kati ya Asasi za Kiraia na taasisi za kiserikali nchini ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, wadau tutakaofanya nao kazi kupitia mradi huu ni Watetezi wa Haki za Binadamu, Mitandao ya kitaifa ya Taasisi za Haki za Bindamu kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utwala Bora (CHRAGG), Mamlaka za Serikali, Watunga sera, Mamlaka za usimamizi wa sheria kama vile Mahakama, Wanasheria, Asasi za Kiraia pamoja na Mashirika yanayotetea Haki za Binadamu, Familia na Jamii wanazoishi Watetezi na Umma wa watanzania kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa, kwa miaka mingi sasa, THRDC imekuwa ikisisitiza juu ya uwepo wa mahusiano mazuri kati ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Taasisi za kiserikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), kwakuwa yana manufaa makubwa kwa maendeleo ya taifa na ni chachu ya ulinzi wa haki za binadamu nchini.

 

Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Aprili 9, 2020