Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa akiwa na Mratibu wa kanda ya Pwani ya Kusini Bw. Clemence Mwombeki, Pamoja na Afisa dawati la Wanachama THRDC Bi. Lisa Kagaruki hii Leo wametembelea Ofisi za Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Abdallah Mohamed Malela.

Mkutano huu wa THRDC na Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara umelenga zaidi kufahamiana kwa Serikali na wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) waliopo katika Mkoa wa Mtwara na namna wanaweza kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Katika ziara hiyo mratibu kitaifa wa THRDC alipata wasaha wa kuutambulisha Mtandao na kazi unazofanya katika kuwawezesha wanachama wake kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na zaidi ni namna Mtandao umeweza kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuandaa kitini kinachotoa mwongozo wa ulipaji kodi kwa AZAKI ili kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Mratibu Kitaifa THRDC amefanikiwa kuelezea namna AZAKI zimejipanga kuendelea kufanya kazi kwa kuoanisha miradi yake na mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano kama ilivyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pindi alipokuwa katika mkutano mkuu wa wadau wa Asasi za Kiraia kilichoandaliwa na Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO ) jijini Dodoma Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, Katibu Tawala wa mkoa, Bw. Malela amekiri kufurahishwa na ugeni wa Mtandao wa THRDC katika ofisi zake na kueleza kuwa wadau wa AZAKI ni watu muhimu katika kuisaidia serikali kutimiza majukumu yake kwa jamii na hata kupitisha baadhi ya ajenda ambazo kwa wakati mwingine zingechukua muda mrefu kufanikishwa na Serikali.

“Tunashukuru sana hatuna mahusiano ya kihasama, tunafanya kazi pamoja na tutaendelea kufanya Kazi pamoja” Abdallah Mohamed Malela, RAS Mtwara

Ameongeza Kuwa…

“Wote tunahitajiana, Serikali haiwezi kutoa maagizo tu kwani mara nyingi kunakosekana utekelezaji, hivyo tunajua taasisi kama hizi zinaturahisishia ufanyaji kazi kwa upande wa Serikali. Kwa level ya mashirika kama haya mara nyingi huelewa nini kinatakiwa, hivyo hupeleka kwa wananchi, na wakati mwingine wananchi wanaweza wasimuamini mkuu wa mkoa, wasiniamini mimi RAS, na hata waziri, lakini anapokwenda mtu wao ambaye siku zote wapo nae, na kutoa ufafanuzi wa kuelezea hili lipo hivi na hili lipo vile na wakakubaliana. Inasaidia jambo kufanyika kwa wepesi ndio maana mi nasema mafanikio yetu ni kwa sababu wenzetu (Asasi za Kiraia) wanatusaidia na tupo tayari kuwa pamoja na kufanya kazi za wananchi.” Abdallah Mohamed Malela, RAS Mtwara

THRDC imetembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Kuzungumza na Katibu Tawala wa Mkoa pindi Mratibu Kitaifa wa THRDC akiwa ziarani mkoani Mtwara alipokwenda kuwatembelea wanachama wa Mtandao walio katika Kanda ya Pwani ya Kusini.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
18 October, 2021