Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa akiwa na Mratibu wa kanda ya Pwani ya Kusini, Bw. Clemence Mwombeki, Mwakilishi kutoka Mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mtwara (MTWANGONET), Bw. Deo Makoti, Pamoja na Afisa dawati la Wanachama THRDC, Bi. Lisa Kagaruki hii leo wametembelea ofisi za mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Dunstan Kyobya.

Mkutano huu wa THRDC na mkuu wa Wilaya umelenga zaidi kujitambulisha pamoja na KUBORESHA mashirikiano baina ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Kanda ya Kusini na Serikali ambazo kwa pamoja zinafanya kazi ya kuisaidia jamii katika maeneo mbali mbali.
THRDC imetembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya pindi wakiwa ziara ya Mratibu Kitaifa mkoani Mtwara alipokwenda kuwatembelea wanachama wa Mtandao walio katika Kanda ya Pwani ya Kusini.

Hata hivyo Mratibu THRDC alipata wasaha wa kuelezea azma kufungua Ofisi ya Mtandao kwa Kanda ya Pwani ya Kusini ambayo itafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali Ili kuendelea kuboresha utolewaji wa huduma kwa wanachama wa Mtandao na jamii kwa ujumla. Ofisi hii itaongeza umoja wa wanachama kwa kuwaleta karibu na kuwaongezea uwezekano wa upatikanaji fursa mbalimbali, shughuli za pamoja za AZAKi, kurahisisha ufikiwaji wa pamoja wa wanachama/AZAKI na serikali yao.

Pia THRDC imeomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na AZAKI zilizopo katika mkoa wa Mtwara Ili kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa Asasi hizo kusaidiana na Serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Dunstan Kyobya alipata wasaha wa kuukaribisha Mtandao Kanda ya Pwani ya Kusini na kuelezea namna Serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na shirika mwanachama wa Mtandao na mratibu wa kanda, Door of Hope pamoja na wanachama wengine mkoani humo katika masuala mbalimbali ya usaidizi wa jamii, uelimishaji na utetezi wa Haki za Binadamu kwa ujumla.

Mwisho, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na THRDC ziliazimia kuendeleza mashirikiano baina yao ambayo kwa kiasi kikubwa yanalenga kujenga nyumba moja (Tanzania), inayothamini, kukuza, kulinda na kuheshimu Haki za Binadamu.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
October 18, 2021