THRDC NA UNIC WAADHIMISHA KUMBUKIZI YA WAHANGA WA MAUAJI YA WAYAHUDI KIPINDI CHA VITA YA PILI YA DUNIA

Dar es Salaam – Tanzania

Asubuhi ya leo tarehe 12 Februari 2020, kwa mara nyingine tena, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ukiwakilishwa na James Laurent – Associate Protection Officer: Research & Documentation, kwa kushirikiana na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa nchini (United Nations Information Centre – UNIC) ikiwakilishwa na Bi. Stella Vuzo – Afisa Habari Kitaifa wa UNIC, kwa pamoja tuliandaa mkutano wa kuwaelimisha vijana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Oysterbay iliyopo jijini Dar es Salaam kuhusu historia ya mauaji ya zaidi ya Wayahudi milioni 6 barani Ulaya, waliouawa na wajerumani kati ya mwaka 1941 hadi mwaka 1945 katika utawala wa waNazi waJerumani chini ya uongozi wa Dikteta Adolf Hitler (1933 – 1945).

Kumbukizi ya Wahanga wa Mauaji ya Wayahudi (The Holocaust):
Kila tarehe 27 Januari, Umoja wa Mataifa (United Nations) pamoja na mataifa wanachama ikiwemo Tanzania, huadhimisha Siku hii ya Kumbukizi ya Wahanga wa Mauaji ya Wayahudi waliokuwa wakiishi barani Ulaya kipindi cha Vita ya pili ya Dunia (the Holocaust); waliouawa na Wajerumani kwa chuki na ubaguzi kisa wao ni Wayahudi.

Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa wanachama wake, kwa heshima ya wahanga hawa waliotoroka katika kambi za mateso mnamo tarehe 27 Januari 1945, huadhimisha siku hii kila mwaka. Mwaka huu, UNIC na THRDC tumeungana kuiadhimisha siku hii leo pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Oysterbay .

Historia ya Mauaji haya ya Wayahudi zaidi ya milioni 6, ni idadi kubwa ya mauaji ya halaiki kuwahi kutokea duniani. Mauaji kama haya yamewahi kutokea pia nchini Rwanda mnamo mwaka 1994 (kati ya Wahutu na Watusi) ambapo zaidi ya watu milioni moja wanadaiwa kuuawa, chanzo chake pia kikiwa chuki na ubaguzi wa kikabila kati ya makabila hayo mawili.

Pia kupitia mkutano huu, James Laurent kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) amewaeleza wanafunzi kuwa wao kama vijana wana jukumu kubwa la kutetea haki za binadamu na kuenzi amani na umoja wa kitaifa kama tunu alizotuachia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

[envira-gallery id=”5891″]