Mratibu taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC Onesmo Olengurumwa, Pamoja na Mratibu THRDC Zanzibar Bw. Abdallah Abeid wametembelea Ofisi za Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) Pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo visiwani Zanzibar.

Katika Ziara hiyo Waratibu THRDC wamekutana na Kamishna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar Bw. Juma Bakari Hassan pamoja na Afisa Mwandamizi Elimu na huduma kwa walipa Kodi Dr. Shuweikha Salum Khalfan, kwa lengo la kukuza mashirikiano baina ya Mtandao na Mamlaka hiyo lakini pia kuiomba Mamlaka ya mapato (TRA) kushiriki katika Mafunzo ya Kodi Kwa Asasi za Kiraia yanayotarajiwa kufanyika mapema mwezi Novemba mwaka huu visiwani humo.

Katika Mafunzo hayo, Mtandao umeialika? Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Pamoja na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kusaidia katika kufanya mawasilisho, kusimamia mijadala Pamoja na kuweka mikakati ya Pamoja ya namna ya kuelimisha na kuendeleza mashirikiano zaidi baina ya Mamlaka hizi na Asasi za Kiraia Nchini huku Kamishna wa Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA), Bw. Juma Bakari akikubali kuwa Mgeni Rasmi katika Mafunzo hayo ikiwa ni hatua muhimu kwa Asasi za Kiraia na Mamlaka hiyo kuendeleza mashirikiano, pamoja na kuchangia maendeleo ya Nchi kupitia ulipaji Kodi. Hatua hii ni mwendelezo wa jitihada za Mtandao zilizoanzia Tanzania bara katika kuwaelimisha wanachama Pamoja na Asasi za Kiraia (AZAKI) juu ya Kodi zilizowekwa na Mamlaka za Mapato Nchini Tanzania Ili kwa kushirikiana na Mamlaka hizi itolewe elimu itakayowawezesha wanachama wa Mtandao Pamoja na Asasi za Kiraia kwa ujumla kulipa Kodi zikiwa na uelewa wa Kutosha wa Kodi wanazotakiwa kulipa kwa serikali kwa maendeleo ya Nchi ya Tanzania.

Imetolewa na

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Octoba 27,2021.