TGNP YARATIBU TAMASHA LA 14 LA JINSIA KUSHEREHEKEA MIAKA 25 YA AZIMIO NA MPANGO KAZI WA BEIJING

Dar es Salaam – Tanzania

Zaidi ya wanaharakati 1000 wa Haki za Wanawake nchini wamekutana leo tarehe 24 Septemba 2019, jijini Dar es Salaam – Tanzania, kwa siku 3 kushiriki Tamasha la 14 la Jinsia linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP-Mtandao).

Pichani ni baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake kwenye tamasha hilo wakibeba mabango yenye jumbe tofauti za kutetea haki za wanawake na kupinga unyanyasaji wa kijinsia.

Aidha, katika ufunguzi wa Tamasha hilo, mgeni rasmi Dr. Gertrude Mongella amewaasa wanawake kuhusu umuhimu wa kuwachagua viongozi wanaojali maslahi ya wanawake katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.

“Chagueni viongozi wanaoweka na kutekeleza ajenda ya wanawake kwenye Ilani yao ya uchaguzi. Wanawake hatutaki kuwezeshwa kwa sababu tunaweza. Tunachotaka ni vikwazo kuondolewa katika kila hatua…Kama ni mawe au kokoto na miba tusaidie kuviondoa tusonge mbele. Tanzania ya viwanda hatajengwa kwa maji yanayochotwa na wanawake kwenye ndoo na nishati ya kuni zinazokatwa na wanawake na kubebwa kichwani. Katika harakati hizi wanawake tunapaswa kuwashirikisha wanaume, na wao wakumbuke kwamba tumewazaa na hatuwezi kuwaacha nyuma. Wanawake tuwajengee uwezo vijana wa kiume watambue mchango wa wanawake katika jamii na pia waungane na vijana wa kike katika kuijenga nchi yetu.”, alisema Dr. Gertrude Mongella.

Pia, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg. Dr. Faustine Ndugulile ambaye amealikwa kama mgeni maalum katika ufunguzi wa tamasha hilo amesema, “Ukatili wa Kijinsia umekithiri nchini. Takwimu zinaonesha kuwa kutoka Januari hadi Desemba 2017 kulikuwa na matukio 41,000 ya ukatili wa kijinsia. Hatuwezi kuendelea kama nchi bila kutatua suala la ukatili wa kijinsia…Tanzania tumepiga hatua kubwa. Tulikuwa na Spika mwanamke na Makamu wa Rais mwanamke.

Maombi yangu:

1) Tukemee ukatili wa kijinsia. Tuvunje ukimya. Tusiwafiche wanaotenda uovu huo…Wengi ni wanafamilia na mara nyingi huishia kwenye familia bila kupeleka shauri kwenye vyombo vya kisheria.

2) Wanawake mjitokeze zaidi kwenye uchaguzi, mgombee nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa.

3)Wanawake muendelee kushikamana. Mnaweza…”

Wageni maalum wengine waliohudhuria ufunguzi wa tamasha hili la 14 la Jinsia ni pamoja na Mama Anna Makinda – Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji mstaafu Sinde Warioba, Mhe. Anders Sjoberg – Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mwakilishi wa UN Women nchini – Bi. Hodan Addou na Bw. Francis Uhadi – mwakilishi wa Foundation for Civil Society.