TAMKO KUHUSU UKIUKWAJI WA SHERIA NA TARATIBU KATIKA KUKAMATWA NA KUSHIKILIWA KWA MWANDISHI ERICK KABENDERA

Utangulizi

Erick Kabendera ni mwandishi wa habari za uchunguzi wa kujitegemea anayeandika kuhusu habari za ndani ya nchi na za Kimataifa. Erick Kabendera alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi tarehe 29 Julai 2019 saa 12 jioni nyumbani kwake Mbweni, wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambapo walivamia nyumba yake na kuondoka naye.

Kwa mujibu wa maelezo ya mke wake na jirani zake, gari iliyotumika kumchukua haikuwa na namba za polisi na ilikuwa imesajiliwa kwa namba T746 DFS. Rekodi ya kamera za CCTV zinaonyesha watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi walimkamata na kuondoka naye nyumbani kwake.

Mke wake alieleza kuwa kundi la watu sita waliojitambulisha kuwa ni askari polisi ambao hawakuvaa sare, walifika na gari na kuizingira nyumba yake kwa zaidi ya saa tatu, kuanzia saa tisa alasiri hadi saa kumi na mbili jioni. Baadaye Bw. Erick Kabendera alikamatwa kwa maelezo kuwa wanampeleka kituo cha polisi cha Oysterbay.

Kabla ya kukamatwa kwake, simu zake za mkononi zilikuwa hazipatikani na laini za simu zilikuwa hazifanyi kazi. Alipiga simu mtandao wa Vodacom kuulizia ambapo alijibiwa kuwa wamepokea maagizo kutoka katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzuia kadi zake za simu. Inasadikiwa kuwa sababu za kuzimwa kwa simu zake ni kwa kuwa alikuwa anawasiliana na majirani na viongozi wa Mtaa kuhusu uwepo wa gari lisiloeleweka getini kwake baada ya kuwachunguza kupitia CCTV.

Utata wa aliposhikiliwa Erick Kabendera kabla ya ndugu kumwona

Mwanzoni maafisa wa polisi katika kituo cha Oysterbay na kituo Kikuu cha Kati walikataa kuwa wanamshikilia Erick Kabendera. Baada ya mivutano mingi na kuonesha ushahidi wa kuwa Kabendera amechukuliwa na Jeshi la Polisi, ndipo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwa Erick Kabendera alikamatwa na Jeshi la Polisi na ameshikiliwa kwa mahojiano kuhusu uraia wake.

Jambo hili pia lilizua maswali mengi yaliyosababisha Mtandao uanze mchakato wa kumtafuta Erick kupitia mahakama. Baada ya kushindwa kuwasiliana na Erick Kabendera, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kupitia mawakili wake, ulianza mchakato wa kumuombea dhamana katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mwandamizi Rwizile.

Kabla ya kituo cha polisi alichoshikiliwa kujulikana, Mke wa Bwana Kabendera alizunguka vituo vingi vya polisi akijaribu kumtafuta mumewe lakini hakufanikiwa. Hata hivyo alifanikiwa kukutana na kamanda wa polisi, Lazaro Mambosasa, ambae alimwambia aende Kituo cha Polisi cha Kati mnamo tarehe 31 Julai, 2019 saa 2 asubuhi. Pia Mke wa mwandishi huyo aliripoti kuwa alipokea simu iliyomwamuru kusalimisha hati ya kusafiria ya mumewe na nakala za kitaaluma kwa Waziri wa Mambo ya ndani.

Tabia ya kuwahamisha watu wanaotuhumiwa kutoka kituo kimoja cha polisi kwenda kingine imeongezeka sana sasa. Tatizo hili hufanyika bila taarifa kwa ndugu na hatimaye kuvunja haki za mtuhumiwa na kuzua taharuki kwa umma kuhusu usalama wa mtuhumiwa. Hii inanyima haki ya uwakilishi wa kisheria na kutembelewa na familia. Maafisa wa polisi walikiuka haki hizi kwa kuwa mke hakuweza kumuona mumewe, na mawakili wake hawakuweza kumpata kwa siku mbili mfululizo.

Baada ya kufuatilia kwa kina na nguvu kubwa, tulifanikiwa kujua kuwa Bwana Kabendera yupo katika kituo cha Polisi cha barabara ya Kilwa (Kilawa road), kituo ambacho hakikutajwa hapo awali na maafisa wa polisi.

Zaidi ya masaa 44 yalipita toka Bwana Kabendera akamatwe na kuwekwa kizuizini katika kituo cha polisi ambacho hakikufahamika mara moja, mpaka tarehe 31.07.2019 ilipodhihirishwa kuwa yupo katika kituo cha Polisi cha Barabara ya Kilwa.

Matakwa ya Sheria kuhusu Haki za Watuhumiwa

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (The Criminal Procedure Act, 1985 Cap 20 R.E 2002) imeeleza wazi taratibu za kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kumfungulia mtu mashtaka.

Kwa namna alivyokamatwa, polisi hawakufata taratibu mbalimbali za sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Utaratibu uliokiukwa ni kama ufuatavyo:
1) Mshtakiwa hakujulishwa sababu za kukamatwa kwake.
Kifungu cha 23 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai hakikuzingatiwa. Alipokamatwa hakuambiwa chochote zaidi ya kuwa anapelekwa kituo cha polisi tena baada ya majirani kuzunguka gari na kuhoji ni wapi Kabendera anapopelekwa.

Sababu za kukamatwa kwake zilikuja kuwekwa bayana baada ya siku kadhaa kupita katika mkutano na waandishi wa habari. Huu sio utaratibu sahihi wa kisheria. Mtuhumiwa alipaswa kujua sababu zilizopelekea akamatwe na kushikiliwa katika kituo cha polisi. Alipokamatwa tarehe 29 Julai 2019, polisi hawakutoa sababu za kukamatwa kwake na pia hawakutoa sababu za kuhoji utaifa wake kwa mara ya pili.

Pamoja na tuhuma hizo na mahojiano, idara ya uhamiaji haijatoa taarifa yoyote kuhusu uchunguzi uliofanywa. Badala yake walimkabidhi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi huku ikionekana hakuna tena tatizo la uraia.

Changamoto kubwa ni kuwa, hadi sasa Idara ya uhamiaji hajamtangaza Erick kuwa sasa ni raia halali na pasi za kusafiria za Erick na familia yake bado pia wanazishikilia. Ikumbwe suala la uraia ndio lililokuwa kosa la kwanza alilitohumiwa nalo Erick Kabendera baada ya kukamatwa.

2) Kufikishwa mahakamani ndani ya wakati uliowekwa kisheria.
Kifungu cha 32(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema kuwa:
“Wakati mtu yeyote amewekwa mahabusu kwa kosa bila kibali, isipokuwa kwa kosa linaloadhibiwa kwa kifo, afisa msimamizi wa kituo cha polisi ambako ameletwa, katika jinsi yoyote, na kama inaonekana haiwezekani kumpeleka mbele ya mahakama inayofaa ndani ya saa ishirini na nne kuanzia alipowekwa mahabusu, anaweza kuichunguza kesi na, isipokuwa kama kosa linaonekana na afisa huyo kuwa ni kubwa, kumwachia mtu huyo baada ya kuweka dhamana kwa kiasi cha kutosha akiwa na wadhamini au bila ya wadhamini, na kumtaka kuhudhuria mbele ya mahakama katika muda na mahali palipotajwa kwenye dhamana; lakini kama atashikiliwa mahabusu atalazimika kupelekwa mbele ya mahakama haraka iwezekanavyo.”

3) Haki ya kuwa na wakili na kuonana na ndugu au rafiki kipindi cha kuchukua maelezo ya mshatakiwa.
Kifungu cha 54 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai mwaka 1985, kinaeleza kuhusu haki ya msingi ya mshtakiwa kuonana na wakili na ndugu wa karibu. Katika haki ya kuonana na mwanasheria wake au mtu wake wa karibu au familia, mwandishi huyu, hapo mwanzoni amehojiwa bila kuwa na wakili wake au mtu wake wa karibu kinyume na utaraibu uliopo kisheria. Haki hii imeshindwa kutekelezeka kwa sababu hapo awali mawakili na familia yake ilishindwa kuwepo wakati akitoa maelezo kwa sababu haikujulikana yupo katika kituo gani cha polisi.

4) Kutokuwa na hatia mpaka itakapothibitishwa.
Ibara ya 13 (6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa, ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kudhaniwa ametenda kosa hilo mpaka pale itakapothibitika ametenda kosa hilo.

Ukiangalia jinsi alivyokamatwa, inaonekana wazi kuwa maafisa wa polisi waliohusika walienda mbele zaidi na kumdhania Bwana Kabendera kuwa na hatia kabla haijathibitishwa na mahakama.

5) Kubadilishwa mashtaka zaidi ya mara tatu ndani ya siku 5.
Jambo lingine lililoonesha uonevu kwa Erick na ukiukwaji wa Sheria ni dhamira ya kulazimisha kumkuta Erick na tuhuma hata ambazo hazikuwa msingi wa kukamatwa kwake. Tukio la kukamatwa, kuhojiwa, limehusisha tuhuma kuu tatu (Uraia, Taarifa za Uongo na Uchochezi) kabla ya kufikishwa mahakamani kwa tuhuma nyingine tatu (Utakatishaji fedha, Kutokulipa Kodi na kushiriki mtandao wa uhalifu).

a) Kuhojiwa kuhusu Uraia
Baada ya kukamatwa kwa mara ya kwanza Bwana Erick alihojiwa na maofisa wa uhamiaji kuhusu uraia wake. Ni vyema ikumbukwe hii ni mara ya pili mwandishi huyu kukamatwa na kuhojiwa kuhusu uraia wake.

Mnamo mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, alitoa tamko la kuondoa utata juu ya madai ya kuwa Bw. Kabendera sio Mtanzania, alieleza kuwa ni Mtanzania na hata wazazi wake ni watanzania.

Vilevile kauli iliyotolewa na Afisa wa Uhamiaji kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ilisema kwamba uraia wa mwandishi huyu pamoja na wazazi wake haukuwa na utata wowote. Waziri huyo aliagiza kuwa maafisa wawili wa uhamiaji waliomkamata na kumhoji juu ya uraia wake waadhibiwe kwa kumdhalilisha yeye pamoja na familia yake.

Mnamo mwaka 2013, Mkurugenzi wa Malalamiko katika Idara ya Uhamiaji, Bwana Augustine Shio, alisema kwamba zoezi lote la kufatilia na kuamua utaifa wa Kabendera pamoja na wa wazazi wake halikuwa sahihi na halikushughulikiwa kitaaluma. Alifafanua kwamba uraia na utaifa wa Erick Kabendera na ule wa familia yake haukuwa na shaka yoyote.
Kufuatia kauli hizo za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Afisa wa Uhamiaji, kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu sababu za kumkamata kwa mara ya pili ikiwa walishathibitisha kuwa ni Mtanzania. Na kama si Mtanzania ni raia wa wapi?.

b) Kuhusu tuhuma za Uchochezi
Baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa na maofisa wa Uhamiaji, Bwana Erick alishikiliwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma za uchochezi mitandaoni. Tuhuma hizi zilihusishwa na nakala yake aliyoitoa kwenye jarida la “The Economist” lililochapishwa tarehe 31 Julai 2019. Hata hivyo tuhuma hizo za uchochezi na utoaji wa taarifa za uongo zilibadilishwa tena pale alipofikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mengine matatu.

c) Tuhuma za kushindwa kulipa kodi, kupanga njama ya kutenda uhalifu na utakatishaji fedha
Wakati mahojiano yakiendelea, makazi ya Bwana Erick Kabendera yalikaguliwa mara kadhaa. Mara ya mwisho katika kukagua nyumba yake, askari polisi waliamuru awapatie hati ya nyumba, kadi za benki na magari. Erick Kabendera aliwasilisha nyaraka alizokuwa nazo kwa muda huo na alitoa ushirikiano wa kukamilisha uwasilishwaji wa baadhi ya nyaraka ambazo hazikuwepo ndani kwa wakati ule, alitoa maelekezo ya wapi vinaweza kupatikana.

Baada ya vuta nikuvute ndani ya siku 6 mfululizo za jitihada za kumuombea dhamana bila mafanikio, hatimaye siku ya 7 mnamo tarehe 5 Agosti 2019, polisi walimpeleka Erick Kabendera Mahakamani. Mawakili walikuwa wamejiandaa kwa kusikilizwa kwa ombi la kupatiwa dhamana kwa kuwa mpaka muda huo hakuwa amefunguliwa shitaka yoyote.

Mwandishi wa habari za kiuchunguzi Erick Kabendera alipofikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu alisomewa mashtaka matatu ikiwemo kushindwa kulipa kodi, kupanga njama ya kutenda uhalifu na utakatishaji fedha. Makosa anayotuhumiwa nayo Erick Kabendera hayana dhamana kwa mujibu wa sheria na hivyo mwandishi huyo anabakia kuwa mahabusu hadi uchunguzi wa kesi yake utakapokamilika na kesi yake kusikilizwa katika Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Sheria hizi za Uhujumu Uchumi na Utakatishaji fedha ni moja ya sheria kandamizi zinazoonekana kwa sasa kukiuka sana haki za watuhumiwa za kupata dhamana, lakini pia haki ya kusikiliziwa mahakamani kwa wakati.

Ni kinyume na haki za binadamu kumkatama mtu ambaye uchunguzi wa awali haukujitosheleza kumtia hatiani. Makosa haya hufanya watu wakae mahabusu kwa miaka mingi bila mashauri yao kusikilizwa. Hivi karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma alishauri watu wasikamatwe hadi pale uchunguzi utakapokuwa umefikia kiwango cha kuridhisha. Erick alibadilishiwa makosa dakika za mwisho. Swali linabaki, walipata muda gani kufanya uchunguzi wa kutosha kumshitaki Erick kwa makosa haya makubwa ambayo hayakuwa makosa ya awali wakati wa ukamataji.

Katika kipindi hiki ambapo Jumuiya za Kimataifa zinafuatilia kwa ukaribu masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini, suala la kukamatwa na kushtakiwa kwa Erick Kabendera limeleta taswira mbaya ya nchi yetu. Balozi mbalimbali zimeshatoa matamko kuonyesha masikitiko yao kuhusu hali ya haki za binadamu na namna ambavyo watuhumiwa kama Erick wamekua wakivunjiwa haki zao kabla ya kupelekwa mahakamani.

WITO WETU:
a) Kutokana na ukweli kwamba awali Bwana Erick alihojiwa kuhusu uraia wake na maofisa wa Uhamiaji kabla ya kubadilishiwa tuhuma, tunawasihi maofisa wa uhamiaji watoe tamko kwamba Erick ni Raia wa Tanzania au vinginevyo kwa mujibu wa uchunguzi wao;

b) Tunashauri pia suala la uraia lisitumike kama silaha ya kuwanyamazisha Watanzania wanaopenda kuhoji mambo ya msingi ya kitaifa;

c) Tunawaomba maofisa wa uhamiaji wamrudishie Bwana Erick, Mke na Watoto hati zao za kusafiria ikiwa hawakuthibitisha kuwa Bwana Erick si raia wa Tanzania;

d) Tunalisihi Jeshi la Polisi kufuata utaratibu katika kukamata watu, ikiwemo kuwataarifu sababu za kukamatwa, ndugu wafahamu kituo cha polisi alichopelekwa na kushikiliwa ili kuepuka sintofahamu na kudhaniwa kuwa mtu ametekwa kumbe amekamatwa na vyombo vya usalama;

e) Maofisa wa jeshi la Polisi watoe haki zote za mshatakiwa kama kuonana na mwanasheria pamoja na familia yake pindi wanapokua wanawashikilia watuhumiwa;

f) Maofisa wa Jeshi la Polisi wajiepushe na vitendo vinavyoweza kuashiria ukiukwaji wa haki za watuhumiwa kama uteswaji au udhalilishaji wa namna yoyote;

g) Polisi wahakikishe wanawapeleka washtakiwa mahakamani ndani ya muda uliowekwa kisheria;

h) Wito kwa wanasheria wote nchini kutafakari na kuchukua hatua ya kupinga sheria ya utakatishwaji fedha na uhujumu uchumi haswa katika suala la dhamana;

i) Katika kipindi hiki ambacho serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, inapitia upya Mfumo wa Haki Jinai nchini, wanasheria na Watetezi wa Haki za Binadamu kote nchini wanapaswa kupinga nguvu na mamlaka makubwa aliyopewa mwendesha mashtaka wa serikali (DPP) katika kuendesha kesi hizi na haswa katika upatikanaji wa vielelezo na ushahidi mbalimbali katika mashtaka ya aina hii;

j) Makosa yote yawe na dhamana. Sheria zote zinazominya haki ya watuhumiwa kupata dhamana zifanyiwe marekebisho ili kuwapa watuhumiwa haki yao ya kuwa huru wakati vyombo vya usalama vinapoendelea na uchunguzi au Mahakama inapoendelea na kesi.

k) Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lipitishe sheria itakayoruhusu makosa yote yawe na dhamana.

l) Mahakama ipewe mamlaka ya kutoa maamuzi kuhusu dhamana. Sheria zisizuie dhamana bali mahakama iamue kuhusu dhamana ya mtu kulingana na mazingira na uzito wa shauri.

m) Masharti ya dhamana katika mahakama zetu na Jeshi la Polisi yalegezwe ili kuweka masharti nafuu yatakayowawezesha watuhumiwa kupata haki yao ya dhamana.

n) Jeshi la Polisi na vyombo vyote vinavyohusika na utoaji haki visikamate watuhumiwa kabla ya kumaliza upelelezi. Tunaungana na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Juma, kuhakisha watu hawakamatwi hadi pale uchunguzi wa kutosha uwe umefanyika. Hii itapunguza muda mwingi wa watuhumiwa kukaa mahabusu.

o) Sheria itamke wazi kwamba ikifika kipindi fulani cha muda na upelelezi haujakamilika basi kesi ifutwe.

p) Tunapendekeza kuwepo utaratibu wa polisi kupeleka shauri la kusikiliza ushahidi (Evidential Hearing). Hii itasaidia upatikanaji wa haki na kwa wakati. Katika mchakato huu polisi wanatakiwa kuleta shauri hilo wakiwa na vielelezo vyote na ushahidi wote mbele ya mahakama. Mahakama isikilize na mtuhumiwa ajibu ndipo mahakama ikiridhishwa kuwa mtuhumiwa ana kesi na anaweza kutiwa hatiani itoe amri ya kukamatwa mtuhumiwa. Shauri hili litasaidia kupunguza muda ambao polisi wanatumia kufanya upelelezi huku mtuhumiwa akinyimwa haki zake za msingi ikiwa kudhaniwa hana hatia mpaka atakapokutwa na hatia, vilevile ushahidi ukiwa umekamilika kesi itaendelea kwa haraka na haki itapatikana.

#FreeErickKabendera

Imetolewa leo tarehe 11/08/2019

Na:

——————————————–
Onesmo Olengurumwa,
Mratibu Kitaifa,
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

————————————
Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji,
Media Council of Tanzania (MCT)

————————————-
Deogratius Nsokolo
Rais,
Union of Tanzania Press Clubs (UTPC)

———————————–
Deodatus Balile
Makamu Mwenyekiti,
Tanzania Editors Forum (TEF)