TAMKO KUHUSU MATUKIO YA KUPOTEA/KUTOONEKANA NA KUTEKWA KWA WATU NCHINI
 
1.0 Utangulizi
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu matukio mbali mbali ya utekaji ambayo yamekuwa yakihatarisha hali ya usalama na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi. Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe Kangi Lugola, mnamo tarehe 14 mwezi Oktoba mwaka 2018 jumla ya matukio 75 ya utekaji yaliripotiwa tangu mwaka 2016. Hata hivyo kulingana na taarifa hizo za Wizara na taarifa zingine, ikiwemo taarifa zilizokusanywa kutoka vyombo vya habari, kuanzia mwaka 2016 mpaka mwezi Julai 2019 jumla ya matukio 86 ya utekaji yaliripotiwa. Kati ya waliotekwa watoto ni 23 na watu wazima ni 63. Kati ya hao 86 wengine wamerudi, wengine wamekutwa wamekufa na wengine hawajulikani walipo hadi sasa.
 
Kutokana na takwimu hizi; inaonekana miaka ya nyuma idadi kubwa ya watu waliokuwa wakitekwa na/ama kupotea walikuwa ni watoto. Hata hivyo, matukio ya hivi karibuni ya watu kupotea/kutekwa yameongezeka kwa watu ambao wanaonekana kuwa na mawazo mbadala. Hali hii imedhoofisha juhudi za kupigania haki za binadamu kutokana na hofu iliyotanda nchini kwa kuhofia watekaji pale raia anapotoa mawazo mbadala. Hii ni kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ambayo inampa kila mwananchi haki ya uhuru wa Mawazo. Mwananchi anapokuwa na hofu ya kutoa mawazo yake basi haki zake nyingi za msingi zinakiukwa kwani tunaamini haki ya kwanza ni haki ya kujieleza. Matukio ya utekaji yamekuwa yakiichafua taswira ya nchi yetu ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha hali ya taharuki kwa wananchi.
 
2.0 Makundi ya Watu Mbali Mbali Waliopotea/Kutekwa
Tofautii na idadi kubwa ya wanaotekwa/kupotea miaka ya nyuma kuwa ni watoto, matukio ya hivi karibuni yanaonesha idadi kuwa ya watu wanaopotea/kutekwa ni; Watetezi wa Haki za Binadamu, Waandishi wa Habari, Wafanyabiashara, Wanasiasa na Wasanii.
 
A: WANAHARAKATI/WANASHERIA
(i) Dkt. Steven Ulimboka
Mnamo tarehe 27 Juni, 2012 Dk Steven Ulimboka alitekwa kipindi hicho akiwa kiongozi wa chama cha madaktari nchini Tanzania. Alitekwa nyara, kuteswa kisha kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na watu ambao hawakufahamika. Ikumbukwe kwamba, Dk Ulimboka alikuwa akitetea maslahi ya madaktari wenzake na ndipo alipokumbana na dhahama ya kutekwa na wasiojulikana. Mpaka sasa hakuna taarifa zozote za kiuchunguzi juu wahusika waliohusika na utekwaji wa Dk Steven Ulimboka.
 
(ii) Abdul Nondo
Mnamo tarehe 7 Machi 2018, kiongozi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Omari Nondo alitekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Ubungo – Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa, ambapo aliachwa karibu na kiwanda cha Pareto. Baadae Abdul Nondo aliripoti kituo cha polisi na kisha kugeuziwa mashtaka kwamba ametoa taarifa za uongo kwamba ametekwa. Hata hivyo, kesi ilienda mahakamani na baadae Nondo aliweza kushinda kesi yake dhidi ya Jamhuri.
 
(iii) Maneno Mbunda
Mnamo tarehe 28 mwezi Aprili 2019, Mtetezi wa Haki za Binadamu na Wakili wa TANAPA, ndugu Maneno Mbunda, alitoweka maeneo ya USA River-jijini Arusha kwa zaidi wiki moja bila kujulikana alipo. Taarifa kutoka kwa mke wa Maneno Mbunda pamoja na wanafamilia zilieleza kuwa Maneno Mbunda hajulikani alipo. Baadae; Mkurugenzi wa Mashtaka, ndugu Abdsalom Mganga, alijitokeza hadharani na kusema kwamba Maneno anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma mbalimbali. Ndugu Mganga alijitokeza hadharani baada ya kelele za Watetezi wa Haki za Binadamu kulaani tukio hilo.
Hali hii ya kukamata watu na kukaa vituo vya polisi/vizuizini kwa muda usiowekwa kisheria yamekuwa yakitafsiriwa kama utekaji kwakuwa wanaotekeleza vitendo hivi hata kama ni askari, wamekuwa wanakaa na watuhumiwa muda mrefu kinyume na sheria bila kutoa taarifa kwa ndugu au jamaa wa mtuhumiwa.
 
(iv) Steven Mussa Ngowo
Mnamo Tarehe 19.02.2019, Mtetezi wa Haki za Binadamu, Steven Mussa Ngowo alitekwa na watu wasiojulikana kasha kuteswa na kutelekezwa huko Mkoa wa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga. Alitoweka kwa siku nne mfululizo. Kisa cha kutekwa kwa ndugu Steven ni kutokana na kuwa na majibizano na Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi, juu ya masuala mbali mbali yahusuyo jimbo hilo na Tanzania kwa ujumla.
 
(v) Wakili Philbert Gwagilo
Mwezi Machi mwaka 2015, taarifa ilitoka ya kupotea kwa Wakili Philbert Gwagilo ambaye ni mwenyeji wa Dodoma. Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa hiyo kilieleza kuwa Gwagilo alipotea katika mazingira ya kutatanisha,huku kukiwa hakuna mwenye taarifa kuhusu wapi Ndugu Philbert Gwagilo amekwenda au amepotelea. Ni zaidi ya miaka minne sasa, Gwagilo hajulikani alipo na hakuna taarifa zozote za kiuchunguzi za kubainisha alipo.
 
B: WANASIASA
(i) Ben Saanane
Mapema mwaka 2017, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ndugu Ben Saanane, alitekwa na Watu wasiojulikana na hakuna taarifa zozote za kiuchunguzi juu na wahusika wa tukio hilo. Ni takribani zaidi ya miaka miwili sasa Ben Saanane hajapatikana na hakuna yeyote aliyekamatwa na/au kushukiwa kuhusika kumteka Ben.
 
(ii) Joseph Kanguye
Ndugu Joseph Kanguye alikuwa ni diwani wa Kata ya Kibondo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Alitekwa na watu wasiojulikana mapema mwaka jana na hakuna taarifa za kupatikana kwake wala taarifa za uchunguzi dhidi ya tukio la kutekwa kwake.
 
(iii) Mdude Nyagali (Maarufu Mdude CHADEMA)
Mdude Nyagali ni kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na mkosoaji mkubwa wa uvunjifu wa haki za binadamu na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi. Mdude amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kukosoa yale ambayo anadhani yanaenda kinyume na demokrasia an utawala wa sheria. Mapema tarehe 6 mwezi Mei mwaka 2019, Mdude alitekwa na watu wasiojulikana kasha kutoweka nae kwa zaidi ya wiki moja kabla ya kuonekana akiwa hajitambui maeneo ya Nvovu katika mkoa wa Songwe.
 
(iv) Allan Kiluvya
Mnamo tarehe 6 July 2019, Allan Kiluvya ambaye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na msaidizi wa Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje ya wa Serikali ya awamu nne Benard Membe, aliripotiwa kupotea baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia tarehe 7 mwezi Julai 2019. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mussa Taibu alizungumzia tukio hilo, ambapo alisema, ‘‘tumepata taarifa za tukio hilo kutoka kwa ndugu wa Allan, na sisi tunaendelea kulifuatilia kujua ni kwa namna gani alichukuliwa lakini siwezi kusema ametekwa kwa sababu bado hatujathibitisha. ’’ Allan alipatikana siku ya Jumatatu ya tarehe 08.07.2019 mbapo anadai watekaji wake walimpeleka hadi eneo la Njia panda ya Segerea na ndipo alipoomba msaada wa ndugu kumfwata. Hakuna taarifa ya uchunguzi inayoonesha wahusika wa tukio hilo mpaka sasa. Kwa mujibu wa Allan, tukio hilo ameshaliripoti polisi na uchunguzi unaendelea.
 
(C) WAANDISHI WA HABARI
(i) Azory Gwanda
Azory Gwanda alikuwa mwandishi wa gazeti la Mwananchi. Alitekwa Novemba 21 mwaka 2017 akiwa katika eneo la Kibiti Mkoani, Pwani. Gwanda alikuwa mwandishi wa habari hasa kuhusu mauaji ya watu kibiti. Tangu kutekwa kwake, vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vimeripoti kwa kina tukio hilo huku pia watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania wamekuwa wakipaza sauti wakitaka uchunguzi ufanywe kuhusu kutoweka kwa mwanahabari huyo.
 
Hivi karibuni tumepokea taarifa mbili zinazokinzana kuhusu kupotea kwa Azory Gwanda kutoka kwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi.
 
Taarifa ya kwanza ni kuwa Azory Gwanda aliyepotea siku 500 zilizopita amefariki. Waziri amesikika na kuonaka kukiri kuhusu kifo cha Azory Gwanda katika mahojiano na kituo cha televisheni cha BBC jijini London ambapo alihojiwa kwa lugha ya kiingereza kwenye kipindi cha focus on Africa majadiliano yakiwa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari duniani.
 
Alinukuliwa akisema:
‘‘Let me tell you, when you refer to that matter, that was one of the most painful experience that Tanzania went through. In the Rufiji area it is not only Azory Gwanda, Azory who has Dissappeared and Died, more than 10 of our colleagues were shot dead, most of the village leaders of Chama Cha Mapinduzi which is the Ruling Party in Tanzania were killed in Rufiji, we thank God that we have been able to contain that kind of extremism in Rufiji, which is now in Northern Mozambique. Last week 9 Tanzanians were killed in Northern Mozambique, so Azory Gwanda is part of many other Tanzanians who have been killed. The state is not only dealing with the issue of Azory Gwanda but all people who have unfortunately Disappeared and died in Rufiji.”, Prof. Kabudi.
 
Aidha Waziri huyo huyo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha BBC Swahili akihojiwa na Zuhura Yunus kwa lugha ya kiswahili profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Azory Gwanda amepotea.
 
Napo alinukuliwa akisema:
“Niseme kwamba hali ya kibiti ilikua tete, watu wengi wameuawa, tena waliouawa wengi ni polisi, viongozi wa serikali za mitaa wa Chama Cha Mapinduzi, na Azory amepotea.’’, Prof. Kabudi.
Taarifa hizi zinakinzana na kuzua maswali mengi. Kifungu cha 161 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kinaelekeza kua mtu atadhaniwa kuwa amekufa katika kuendesha mashtaka yoyote ya kiraia, jinai na ndoa ikiwa mtu huyo hajasikika wala kuonekana na watu wake wa karibu ambao wangepaswa kujua alipo kwa muda wa miaka 5.. Ikiwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ametoa taarifa hizi mbili zinazokinzana katika nyakati tofauti; tungependa kupata taarifa rasmi kutoka kwake ili familia, waandishi wa habari pamoja na watanzania kwa ujumla wapate taarifa yenye uhakika kuhusu kutoweka kwa Azory Gwanda .
 
Katika kutaka kutaka ufafanunuzi wa kauliz hizi mbili tata, THRDC iliongea na Waziri Kabudi, na katika majibu yake amesisitiza kuwa kauli yake sahihi ambayo angependa umma uusimamie ni ile kauli aliyoitoa katika idhaa ya Kiswahili ya BBC iliyoonekana Waziri kukiri Azori Gwanda kupotea. Hivyo kwa kauli hii ya Waziri baada ya kuongea na THRDC ukweli unabakia kuwa Azori hadi sasa hajulikani alipo na si kuwa amefariki. Tuendelee kupaza sauti Mwandishi Azori apatikane.
 
(ii) Salma Said
Salma ni mwandishi wa habari wa kitaifa na kimataifa wa Radio DW. Alitekwa Machi 18, 2016 katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam baada ya kuwasili akitokea Zanzibar na siku tatu baadaye alikutwa katika Hospitali ya Regency, mjini Dar es Salaam.
 
Salma alipohojiwa na vyombo vya habari, alidai kwamba alitekwa na wanaume wawili baada ya kumkamata na kumuingiza kwenye gari na kuondoka naye kusikojulikana. Alieleza kuwa watu hao walimfunga mtandio wake mweusi usoni ili kumbambaisha asitambue mahali walikokuwa wakimpeleka.
 
(D) WAFANYABIASHARA
(i) Mohamed Dewji
Mfanyabiashara MOHAMED DEWJI, alitekwa Mnamo tarehe 11 Oktoba mwaka 2018 na watu wasiojulikana. Mo Dewji alitekwa alfajiri ya tarehe 11 wakati akiwa mazoezini katika hoteli ya Collossium iliyoko Masaki jijini Dar es Salaam. Awali polisi walikaririwa wakisema watekaji wa Mo Dewji walikuwa ni raia waliokuwa na asili ya kizungu. Hata hivyo baada ya kukaa pasipojulikana kwa takribani siku sita, Mo Dewji alipatikana katika Viwanja vya Gymkana huku gari lililodaiwa kuhusika na kumteka likiwa limetelekezwa katika viwanja hivyo. Mpaka sasa mshukiwa mmoja wa tukio hilo ameshafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
 
(ii) Raphael Ongangi
Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Raphael O. Ongangi alitekwa siku ya Jumatatu Juni 24, 2019 na watu wenye silaha akiwa anaelekea nyumbani kwake maeneo ya Masaki. Raphael alikuwa mshauri wa karibu wa ndugu Zitto Kabwe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Raphael alipatikana Julai 2, 2019 huko Mombasa nchini Kenya.
 
(iii) Samson Josiah
Alikuwa mfanyabiashara wa mabasi Kampuni aina ya Super Sammy. Aliripotiwa kutoweka mnamo tarehe 27 Februari mwaka 2018. Samson Josiah alikutwa ameshashafariki huku mwili wake ukiwa umefungwa kwenye kiroba na kutupwa mtoni. Taarifa za kuonekana kwake zilikuja na wavuvi wa samaki mnamo tarehe 14 Machi mwaka 2018.
 
(E) WANAMUZIKI
(i) Roma Mkatoliki na wenzake watatu
Roma na wenzake watatu walitekwa April, 2017. Tukio la kutekwa nyara kwa msanii wa nyimbo za Hip Hop, Ibrahim Musa maarufu kama R.O.M.A Mkatoliki na wenzake watatu lilifanyika kwenye Studio za Tongwe Records Masaki jijini Dar es Salaam walipokuwa wakifanya kazi ya kurekodi nyimbo.
R.O.M.A mkatoliki kwa muda mrefu amekuwa akiimba nyimbo za kukosoa madhaifa ya serikali. Watekaji hao walifika katika studio hizo majira ya saa 12:30 jioni na kuongea na Roma kwa takribani robo saa na waliondoka saa 12:45 baada ya kumuingiza Roma na wenzake kwenye gari.
 
(ii) Moni Centrozone
Ni msanii wa kizazi kipya ambaye alitekwa wakati anarekodi wimbo wake katika studio za Tongwe zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam. Moni anadaiwa kutekwa pamoja na R.O.M.A April 2017 ambapo hakuonekana kwa takribani wiki moja. Baadae, aliripotiwa kuonekana katika kituo cha polisi cha Oyterbay huku akiwa na majeraha sehemu mbali mbali za mwilini.
 
(iii) Bin Laden
Ni msanii wa kizazi kipya ambaye alitekwa wakati anarekodi wimbo wake katika studio za Tongwe zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam. Bin Laden anadaiwa kutekwa pamoja na R.O.M.A April 2017 ambapo hakuonekana kwa takribani wiki moja. Baadae, aliripotiwa kuonekana katika kituo cha polisi cha Oyterbay huku akiwa na majeraha sehemu mbali mbali za mwilini.
 
 
3.0 Usalama wa Raia na Mali zao Kisheria
Ni lazima ikumbukwe kwamba kila mtu anayo haki ya ulinzi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Vyombo vya dola vina wajibu wa kuwalinda raia na mali zao. Ibara ya 7 ya Azimio Juu ya Ulinzi wa Watu Wote Dhidi ya Upotevu inasema kwamba ‘‘hali yoyote ile, iwe tishio la vita, hali ya vita, migogoro ya kisiasa ndani au nyingine ya dharura ya umma, haiwezi kuhalalisha kupotea kwa mtu’’.
 
Jeshi la polisi nchini linafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Polisi na Huduma Saidizi ya Mwaka 1969, Polisi wana jukumu la kulinda raia na mali zao. Pia katika sehemu ya 2, Kifungu cha 5 (1) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi kinasema; “Jeshi la Polisi litaajiriwa katika Jamhuri yote ya Muungano kwa ajili ya kulinda amani, kudumisha sheria na utulivu, kuzuia na kugundua uhalifu, kuwakamata na kuwaongoza watuhumiwa na kulinda mali, na katika utekelezaji wa majukumu yote hayo watakuwa na haki ya kubeba silaha.” Hii yote ni mamlaka waliyopewa polisi katika kuwalinda raia na mali zao.
 
Tumesikitishwa na ongezeko la watu kutoweka na kwenda pasipojulikana na hakuna chochote kinachofanyika au kuonekana kufanya kuzuia suala hili linalozidi kuota mizizi katika jamii. Makundi ya watetezi, waandishi, wanasiasa na wasanii wamesharipotiwa kupotea na kutoweka. Kati yao wapo waliokotwa wameumizwa vibaya, wapo ambao hadi leo hawajulikana walipo na wengine kurudi wakiwa na hofu kubwa.
 
Jukumu la polisi kulinda raia na mali zao linaambatana na kufanya uchunguzi dhidi ya matukio mbali mbali ya ukiukwaji wa haki za raia na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika. Yanapotokea matukio makubwa ya uvunjifu wa haki za binadamu hatua hazichukuliwi, Jeshi letu la polisi linatupa wasiwasi juu ya weledi na utashi wao katika kutekeleza majukumu yao.
 
 
4.0 Kauli za Viongozi Wakuu wa Nchi na Utekelezwaji Wake
Katika kuhakikisha Matukio ya Utekaji yanapungua na ama kuisha kabisa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mnamo tarehe 4 Machi 2019 wakati anahutubia katika hafla fupi ya kuwaapisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Katiba wa Sheria alitoa malekezo juu ya hatua kuchukuliwa hatua dhidi ya wahusika wa utekaji wa Mohamed Dewji. Rais alisema yafuatayo ‘‘Watanzania Si Wajinga. Wanafahamu na wajaua kuchambua mambo. Alipotekwa Mo tulipata stori nyingi. Lakini lilipokuja kumalizika lile suala, kila mtu anajiuliza maswali. Eti Mo Dewji amepatikana Gymkana na silaha zimeachwa pale. Baada ya siku chache tunamkuta aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa. Badae tukaambiwa aliyekuwa dereva wa watekaji amekamatwa. Lakini mpaka sasa kimya. Hizi dosari ndogo ndogo zinalichafuya jeshi la polisi. Nasema kwa dhati kabisa. Wale wachache wanaokwamisha jitihada za jeshi la polisi kufanya kazi yake vizuri ni lazima wachukuliwe hatua. Sasa naomba muende mkachukue hatua. Tukilianzisha swala lazima zimalizike, ili na wengine wajue matokeo yake.’’
 
Ingawa, dereva aliyedaiwa kuwabeba watekaji wa MO Dewji amefikishwa mahakamani, bado watekaji wenyewe hawajaweza kupatikana na hakuna ripoti ya uchunguzi iliyotolewa mpaka sasa.
 
Tunapenda kupongeza jitihada za Rais wetu Dk John Pombe Magufuli katika kuhimiza jeshi la polisi kuchukua hatua za makusudi kuwatafuta watekaji na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Aidha, tunaendelea kumsihi Rais wetu aendelee kufanya hivyo ili watekaji wa raia wengine ambayo hawajulikani walipo hadi sasa na wale waliokwisha onekana waweze kufikishwa mahakamani.
 
Viongozi wetu wengine haswa mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wamekuwa wakitoa kauli za kutia moyo mara tu baada ya kuripotiwa tukio la utekaji/kupotea mtu. Hata hivyo muendelezo wa kauli na utekelezaji wa kauli hizo kwa vitendo imekuwa ni changamoto. Mfano, alipotekwa Ben Saa Nane, Waziri wa Mambo ya Ndani kipindi hicho, Ndugu Mwigulu Nchemba, aliahidi kuagiza kufanyika uchunguzi wa kina kuwatambua watekaji lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote za uchunguzi. Hali kadhalika, alipotekwa Azory Gwanda, ahadi nyingi zilizotolewa na Mawaziri wa mambo ya ndani kwa nyakati tofauti tofauti lakini cha kushangaza nikwamba, mahojiano ya mwisho yaliyofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Sasa, Kangi Lugola, alikaririwa akisema kwamba ndugu Azory Gwanda huenda alitoweka na kwenda anapopajua na sio kwamba ametekwa na hivyo jeshi la polisi halishughuliki na uchunguzi wa kutoweka kwake tena.
 
 
5.0 Wito Wetu
I. Vyombo vya ulinzi na usalama Tanzania vihakikishe kuwa kila raia anaishi kwa uhuru na usalama nchini Tanzania. Jeshi la Polisi liwe tayari kuwalinda raia na mali zao dhidi ya jambo lolote baya.
 
II. Kutokana na wimbi hili la utekaji na kutoweka kwa Watanzania wenzetu, Serikali ya Tanzania inapaswa kutia sahihi na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa kwa Ajili ya Ulinzi wa Watu Wote Waliotekwa na Kuwekwa Vizuini pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Utesaji na Vitendo Vingine vya Kikatili vinavyotweza utu wa Binadamu.
 
III. Serikali ihakikishe wahusika wote wa tukio la kupotea kwa Mwandishi Azory Gwanda, Joseph Kanguye, Philbert Gwagilo, Ben Saanane, na wengine ambao wamepatikana kama vile Mdude Nyagali, Mo Dewji, Roma Mkatoliki, Salma Saidi, Dk Steven Ulimboka wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sehria ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na kukomesha matukio kama haya siku za usoni.
 
IV. Viongozi wa siasa na Bunge waone haja ya kulijadili suala hili la utekajji na kupotea kwa watanzania wenzetu na kuja na maazimio. Tunatamani tukio la kutekwa kwa Allan Kiluvya liwe la mwisho kwa nchi yetu.
 
V. Jeshi la polisi lihakikishe sheria na taratibu za nchi zinafwata pindi raia anapokamatwa na sio kukamata na kukaa na raia kwa muda mrefu bila taarifa hali ambayo inazua taharuki kwa wananchi na kuharibu taswira nzuri ya nchi yetu. Mfano mzuri ni tukio la kutoweka kwa Wakili Maneno Mbunda.
 
VI. Wahanga wa Utekaji au watu wanaopotea na kisha kupatikana, wanapotoka hadharani na kuongea na umma waeleze kinagaubaga kilichowakuta ili kuondoa sintofahamu na ombwe ambalo watanzania, wanahabari linawakumba pale wanapotumia jitihada kubwa kutafuta waliopotea au kutekwa na baadae kutokuongea lolote kwa kigezo cha kwamba polisi wanafanya uchunguzi. Hali hii imesababisha matukio haya kuongezeka na mara nyingi inawakatisha tamaa watanzania na muda mwingine kuanza kufikiria/kuhisi kwamba huenda watu wanaoripotiwa kutekwa au kupotea wengine wanaigiza tu.
 
VII. Wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na watanzania kwa ujumla tuendelee kuimarisha usalama wetu kipindi hichi ambapo wimbi la utekaji limeshamiri nchini.
 
 
Imetolewa leo tarehe 11/07/2019
Na:
Bw. Onesmo Olengurumwa,
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)