TAMKO KUHUSU KUKAMATWA NA KUSHIKILIWA KWA MWANDISHI ERICK KABENDERA

Erick Kabendera ni mwandishi wa habari za uchunguzi wa kujitegemea anaye andika machapisho kuhusu habari za ndani ya nchini na za Kimataifa.  Erick Kabendera alikamatwa na Jeshi la Polisi tarehe 29 Julai 2019 saa 12 jioni nyumbani kwake Mbweni, wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es salaam, ambapo walivamia nyumba yake na kuondoka nae. Kwa mujibu wa maelezo yamke wake na jirani zake, gari ilotumika kumchukua haikuwa na namba za polisi na ilikuwa imesajiliwa kwa namba T746 DFS.

Rekodi ya kamera za CCTV zinazoonyesha watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi walimkamata na kuondoka nae nyumbani kwake.

Mke wake alieleza kuwa kundi la watu sita waliojitambulisha kuwa ni askari polisi ambao hawakuvaa sare walifika na gari na kuizingira nyumba, walimkata Bw. Erick Kabendera kwa madai ya kuwa wanampeleka kituo cha polisi cha Osterbay.

 

Kabla ya kukamatwa kwake, simu zake za mkononi zilikuwa hazipatikani na laini za simu zilikuwa hazifanyi kazi, alipiga kuuliza mtandao wa Vodacom ambao walijibu kuwa wamepokea maagizo kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzuia kadi zake za simu.

 

Baada ya kushindwa kuwasiliana na Erick Kabendera, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kupitia mawakili wake, ulianza mchakato wa kumwombea dhamana katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu mwandamizi Rwizile.

Mara ya kwanza maafisa wa polisi katika kituo cha Oysterbay na na kituo Kikuu cha Kati walikataa kuwa wanamshikilia Erick Kabendera. Baada ya mivutano mingi na kuonesha ushahidi wa kuwa Kabendera amechukuliwa na  Jeshi la Polisi ndipo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwa Erick Kabendera alikamatwa na Jeshi la Polisi na  na ameshikiliwa kwa mahojiano kuhusu uraia wake.  Jambo hili pia lilizua maswali mengi yaliyosababisha Mtandao uanze mchakato wa kuomba dhamana na mshtakiwa afikishwe mahakamani.

Kabla ya kituo cha polisi alichoshikiliwa kujulikana, mke wa Bwana Kabendera alizunguka vituo vyote vya polisi akijaribu kumtafuta  mumewe lakini hakufanikiwa. Hata hivyo alifanikiwa kukutana na kamanda wa polisi, Lazaro Mambosasa, ambae alimwambia aende kituo cha polisi cha Kati mnamo tarehe 31 Julai, 2019 saa 2 asubuhi. Mke wa mwandishi huyo anaripoti kuwa pia alipokea simu  iliyomwamuru kusalimisha hati ya kusafiria ya mumewe na nakala za kitaaluma kwa Waziri wa Mambo ya ndani.

Tabia ya kuwahamisha watu wanaotuhumiwa kutoka kituo kimoja cha polisi kwenda kingine imeongezeka kufuatia mwenendo ambao umeongezeka katika kukamata waandishi wa habari na raia wengine. Hii inanyima haki ya uwakilishi wa kisheria na kutembelewa na familia. Maafisa wa polisi walikiuka haki hizi kwa kuwa mke hakuweza kumuona mumewe, na mawakili wake hawakuweza kumpata.

Kwa sasa tuna uhakika kuwa Bwana Kabendera yupo kituo cha Polisi cha barabara ya Kilwa (Kilawa road), kituo ambacho hakikutajwa hapo awali na maafisa wa polisi.

Zaidi ya masaa 24 yamepita tangu Bwana Kabendera akamatwe na kuwekwa kizuizini katika kituo cha polisi ambacho hakikufahamika mara moja mpaka leo tarehe 31.07.2019 ilipodhihirishwa kuwa yupo katika kituo cha Polisi cha Barabara ya Kilwa.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (The criminal procedure Act 1985 Cap 20 R.E 2002) imeelezea wazi taratibu za kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kumfungulia mtu mashtaka.

kwa namna alivyokamatwa polisi hawakufata taratibu mbalimbali za sheria ya makosa ya jinai. Utaratibu uliokiukwa ni kama ufuatavyo:

  1. Mshtakiwa hakujulishwa sababu za kukamatwa kwake alipo kuja kukamatwa. Kifungu cha 23 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai hakikuzingatiwa. Alipokamatwa hakuambiwa chochote Zaidi ya kuwa anapelekwa kituo cha polisi tena baada ya majirani kuzunguka gari na kuhoji anapopelekwa Kabendera.

Sababu za kukamatwa kwake zilikuja kuwekwa bayana Baadae katika mkutano na waandishi wa habari, ndio jeshi la polisi lilitoa sababu za kumkamata, huu sio utaratibu sahihi wa kisheria.   Mtuhumiwa alipaswa kujua sababu zilizopelekea akamatwe na kushikiliwa katika kituo cha polisi. Alipokamatwa tarehe 29 Julai 2019, polisi hawakutoa sababu za kukamatwa kwake na pia hawakutoa sababu za kuhoji utaifa wake kwa mara ya pili. Idara ya uhamiaji haijatoa taarifa yoyote pia.

  1. Kufikishwa mahakamani ndani ya wakati uliowekwa kisheria, Kifungu cha 32(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema kuwa:

“Wakati mtu yeyote amewekwa mahabusu kwa kosa bila kibali, isipokuwa kwa kosa linaloadhibiwa kwa kifo, afisa msimamizi wa kituo cha polisi ambako ameletwa, katika jinsi yoyote, na kama inaonekana haiwezekani kumpeleka mbele ya mahakama inayofaa ndani ya saa ishirini na nne kuanzia alipowekwa mahabusu, anaweza kuichunguza kesi na, isipokuwa kama kosa linaonekana na afisa huyo kuwa ni kubwa, kumwachia mtu huyo baada ya kuweka dhamana kwa kiasi cha kutosha akiwa na wadhamini au bila ya wadhamini, na kumtaka kuhudhuria mbele ya mahakama katika muda na mahali palipotajwa kwenye dhamana; lakini kama atashikiliwa mahabusu atalazimika kupelekwa mbele ya mahakama haraka iwezekanavyo.

Bw. Kabendera alikamatwa tarehe 29 Julai, 2019, mpaka hivi sasa zimepita siku mbili (2) na bado hajafikishwa mahakamani wala kushtakiwa kwa kosa lolote.

  1. Haki ya kuwa na wakili na kuonana na ndugu au rafiki  kipindi cha kuchukua maelezo ya mshatakiwa ,kifungu cha 54 cha Sheria Ya Makosa ya Jinai mwaka 1985 kinaeleza kuhusu haki ya msingi ya mshatkiwa kuonana na wakili na ndugu wa karibu .Haki ya kuonana na mwanasheria wake au mtu wake wa karibu au familia, mwandishi huyu amehojiwa bila kuwa na wakili wake au mtu wake wa karibu kinyume cha utaraibu uliopo kisheria. Haki hii imeshindwa kuekelezeka kwa sababu hapo awali  mawakili na familia yake ilishindwa kuwepo akiwa natoa maelezo kwa sababu haikujulikana yupo katika kituo gani cha polisi.
  2. Kutokuwa na hatia mpaka itakapothibitishwa.

Ibara ya 13 (6)(b)  ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeeleza kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kudhaniwa ametenda kosa hilo mpaka pale itakapothibitika ametenda kosa hilo .

Kwa namna ya ukamatwaji wake Inaonekana wazi kuwa maafisa wa polisi wanaohusika wameenda mbele zaidi na kumdhania Bwana Kabendera kuwa na  hatia kabla hajathibitishwa kuwa na hatia na kushindwa kumfikisha mahakamani.

Ni vyema ikumbukwe hii ni mara ya pili mwandishi huyu kukamatwa na kuhojiwa kuhusu uraia wake, mnamo mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani, Emmanuel nchimbi, alitoa tamko la kuondoa utata juu ya madai ya kuwa Bw. Kabendera sio mtanzania, alieleza kuwa ni mtanzania na hata wazazi wake ni watanzania.

Vilevile kauli iliyotolewa na afisa wa uhamiaji kwa niaba ya waziri wa mambo ya ndani ilisema kwamba uraia wa mwandishi huyu pamoja na wazazi wake haukuwa na utata wowote. Waziri huyo aliagiza kuwa maafisa wawili wa uhamiaji waliomkata na kumhoji juu ya uraia wake waadhibiwe kwa kumdhalilisha yeye pamoja na familia yake.

Mnamo mwaka 2013, mkurugenzi wa malalamiko katika idara ya Uhamiaji, Bwana Augustine Shio, alisema kwamba zoezi lote la kufatilia na kuamua utaifa wa Kabendera pamoja na wa wazazi wake halikuwa sahihi na halikushughulikiwa kitaaluma. Alifafanua kwamba uraia na utaifa wa Erick Kabendera na ule wa familia yake haukuwa na shaka yoyote.  Bwana Shio alifafanua zaidi kuwa pesa ililipwa kwa maafisa hao wawili wa uhamiaji na chanzo cha nje ili kujua utaifa wa kabendera, lakini jambo hilo halikuwa haramu.

Kufuatia kauli hizo za Waziri wa zamani na Afisa wa Uhamiaji, kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu sababu za kumkamata kwa mara ya pili ikiwa walishathibitisha kuwa ni mtanzania. Na kama si mtanzania ni raia wa wapi?

 

Taarifa zilizotufikia hadi sasa ni kwamba askari wameenda kukagua nyumba yake pamoja na mawakili kutoka Mtandao Wa watetezi Wa Haki Za Binadamu (THRDC).

Hakimu anayesimamia kesi hiyo atasikiliza ombi la dhamana  hiyo kesho tarehe 01.08.2019.

WITO WETU

  1. Tunaliomba Jeshi la Polisi kufuata utaratibu katika kukamata watu , ikiwemo kuwataarifu sababu za kukamatwa, ndugu wafahamu kituo cha polisi alichopelekwa na kushikiliwa ndugu yao ili kuepuka sintofahamu na kudhaniwa kuwa mtu ametekwa kumbe amekamatwa kihalali.
  2. Kutoa haki zote za mshatkiwa kama kuonana na mwanasheria pamoja na familia yake
  3. Haki ya kutokuteswa wala kudhalilishwa kwa namna yoyote
  4. Kupelekwa mahakamani ndani ya muda uliowekwa kisheria

 

 

Imetolewa leo tarehe 31 Julai 2019,

Na:

………………………………

Onesmo Olengurumwa,

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi Wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)