TAMKO KUHUSU KUKAMATWA KWA WAKILI JOSEPH RHOBI MARTINUS

1.0 Utangulizi
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unalaani vikali kitendo cha kukamatwa na kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa Wakili Joseph Rhobi Martinus (Roll No. 7357). Wakili huyo alikamatwa kwa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mnamo tarehe 22.11.2019 ambapo aliachiwa jioni yake na kisha kukamatwa tena leo tarehe 24.11.2019 majira ya asubuhi. Joseph anashikiliwa katika kituo cha polisi Shinyanga.

Taarifa za kukamatwa tena kwa wakili Joseph zimethibitishwa na Wakili Johannes Mbatina ambaye amekuwa akifuatilia sakata la kukamatwa kwa Wakili Joseph. Mpaka sasa, sababu za kukamatwa kwa Wakili Joseph hazijaelezwa. Taarifa zinaeleza kuwa Wakili Joseph amekamatwa tena mara tu baada ya agizo la kuachishwa kazi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na RCO wa mkoa huo. Mpaka sasa wakili huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi na dhamana yake haijaweza kupatikana. Wakili Joseph alikamatwa wakati akiwa anatekeleza majukumu yake ya uwakili ambapo alikuwa anasimamia wateja wake wanaodaiwa kukwepa kodi.

2.0 Kazi ya Uwakili na Haki za Wakili Kisheria
Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 64 cha Sheria ya Mawakili (Advocates Act) wakili ni afisa wa mahakama na anatekeleza majukumu yake ya usimamizi wa wateja mahakamani na mahali pengine kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, tabia ambayo imejengeka ya kuwakamata mawakili na kuwahusisha na makosa ya wateja wanaowasimamia ni kinyume na Katiba na sheria za nchi.

Ikumbukwe pia kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kingenecho kinachohusika. Kwa mujibu wa Ibara hii ya Katiba, haki ya mtu kusikilizwa inahusisha pia haki ya kuwa na uwakilishi katika hatua mbali mbali za utafutaji wa haki. Pia Katiba inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. Kwahiyo, wakili Joseph kuwakilisha mteja wake ni haki yake pamoja na haki ya mteja wake kwa mujibu wa Katiba.

Tabia za kuwakamata mawakili wakiwa wanatekeleza majukumu yao zimekithiri ambapo mwaka jana tulishuhudia kukamatwa kwa Wakili Patricia Ng’mario, Wilson Mafie, Nixon Tugara na mwaka huu alikamatwa Wakili Maneno Mbunda pamoja na wakili Joseph Martinus. Tabia hii si tu inaenda kinyume na sheria bali pia imekuwa tishio kwa taaluma ya uwakili kwani mawakili wamekuwa na hofu ya kutekeleza majukumu yao kwa kuhofia usalama wao.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeshamuweka wakili Johannes Mutabingwa Mbatina ambaye ni kiongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Chapter Convener) kuendelea kufuatilia dhamana ya Ndugu Joseph na tutaendelea kuwahabarisha kadri tutakavyokuwa tunapata taarifa.

3.0 Wito Wetu
• Tunaliomba Jeshi la polisi kumwachia mara moja wakili Joseph Martinus kwa kumpa dhamana kwakuwa ni haki yake kisheria. Endapo kuna kosa lolote alilofanya wakili Joseph basi utaratibu wa kisheria ufuatwe ili aweze kupata haki zake kisheria.
• Tunalisihi jeshi letu la polisi kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na kuacha kutumika vibaya kwa kukamata watuhumiwa na kuendelea kuwashikilia kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
• Mawakili waungane na kuendelea kupigania haki zao na haki za watanzania kwani wanafanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.

 

Tamko hili limetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

Tarehe 24.11. 2019