TAMKO KUHUSU KUKAMATWA KWA WAANDISHI WA HABARI ARUSHA

Jumatatu Machi 23, 2020 Mwandishi wa Habari wa Azam TV Ramadhani Mvungi, Mwandishi Novatus Makunga na Mpiga Picha Mohammed Mkindo ambao wote hufanya kazi Jijini Arusha, Tanzania walikamatwa na askari wa jeshi la polisi baada ya kuingia kwenye eneo lililozuiwa. Eneo hilo ni hoteli ambayo watu wamezuiwa na serikali kuingia kutokana na ukweli kwamba mgonjwa wa kwanza wa virusi vya korona nchini alikaa ndani ya hoteli hiyo kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo. Waandishi hao pamoja na mpiga picha huyo walifikishwa kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kwa ajili ya mahojiano na baadae waliachiwa huru bila masharti yoyote.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unawasihi waandishi wa habari pamoja na wananchi wote kutoingia kwenye maeneo yaliyozuiwa hasa katika kipindi hiki cha uwepo wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona. Wote tunapaswa kutii vizuizi halali vilivyotangazwa na serikali ili kuepuka usambaaji wa virusi hivyo ambavyo ni hatari kwa maisha yetu.

Je, Serikali ina mamlaka kisheria kuzuia baadhi ya maeneo na kuweka watu karantini kwa siku 14?

Ndio, kwa mujibu wa kifungu namba 9 cha Sheria ya Afya kwa Umma ya Mwaka 2009, katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wowote, Afisa wa Afya kupitia notisi ya Waziri wa Afya, anaweza kuzuia watu kwenda kwenye maeneo yenye maambukizi. Sheria inayohusika na masuala ya afya nchini ni Sheria ya Afya kwa Umma ya Mwaka 2009 ambayo kwenye kifungu namba 9 inaeleza kwamba Waziri wa Afya kwa kushauriana na Afisa husika ataufahamisha umma kwa kuchapisha kwenye magazeti, mbao za matangazo kwenye eneo husika au kwa njia nyingine yoyote ambayo itaonekana inafaa kuufahamisha umma juu ya uwepo wa ugonjwa wowote unaoambukizika na usioambukizika.

Kifungu namba 10 cha Sheria ya Afya kwa Umma kinasema; “mtu yeyote anayeugua ugonjwa unaopaswa kutolewa taarifa au unaoambukizika anapaswa kutoa taarifa yeye mwenyewe au kutolewa taarifa na mmiliki wa eneo hilo, ndugu au yeyote anayeishi kwenye eneo hilo kwenye mamlaka iliyopo karibu au kwa Afisa wa Afya wa eneo hilo”. Hiki ndio kifungu kinachotoa mamlaka kisheria ya watu kuripoti uwepo wa virusi vya korona.

Aidha, Sheria inasema kwamba pale ambapo kituo binafsi cha afya kinapopokea au kutibu mgonjwa mwenye ugonjwa unaombukizika, kitapaswa kutoa taarifa haraka kwa Afisa wa Afya wa eneo hilo ambaye atatoa notisi kwa njia ya maandishi kwenye gazeti au sehemu ya wazi juu ya uwepo wa ugonjwa unaoambukizika. Kwa maana hiyo, hakuna mtu anayeruhusiwa kutangaza maambukizi mapya ya korona isipokuwa mamlaka za serikali chini ya Wizara ya Afya, Waziri Mkuu au Rais.

Kifungu namba 12 cha Sheria ya Afya kwa Umma ya Mwaka 2009 kinasema kwamba, mgonjwa yeyote mwenye ugonjwa unaoambukizika anapaswa kutengwa na watu wengine. Pale ambapo Daktari au afisa wa afya muhusika atakapothibitisha uwepo wa ugonjwa au akiwa na sababu za kuamini kwamba mgonjwa ana ugonjwa unaoambukizika ataamuru kuwa mgonjwa huyo atengwe, apelekwe hospitali au kwenye kituo cha afya na awekwe kwenye karantini. Hivyo, imepigwa marufuku kwa mtu yeyote asiyehusika kuingia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matibabu ya watu wenye dalili au virusi vya korona.

Kifungu namba 15 cha Sheria hiyo kinasema kwamba sehemu au eneo lote la Wilaya lenye mlipuko wa ugonjwa wa kuambukizika, Afisa wa Afya wa eneo hilo atatoa utaratibu wa karantini ili kudhibiti mlipuko wa usambaaji wa ugonjwa huo. Taratibu za karantini ni pamoja na zifuatazo;
a) Kuzuiliwa kwa shughuli kadhaa au biashara ambazo zinaweza kuendeleza maambukizi;
b) Kuzuia watu kuingia kwenye nyumba au maeneo yenye watu wenye maambukizi, vituo vya afya au kuvuka mipaka;
c) Kutengeneza vituo vya Matibabu vya muda mfupi;
d) Kuchukua taratibu nyingine yeyote ya usimamizi ili kuzuia mlipuko.

Ni kinyume na sheria kusambaza ugonjwa kwa binadamu wengine. Kifungu namba 16 cha Sheria ya Afya kwa Umma ya Mwaka 2009 kinasema kwamba mtu yeyote ambaye;

a) Anajua kwamba ana ugonjwa unaoambukizika na ana uwezo wa kusababisha maambukizi kwa watu wengine juu ya uwepo wake kwenye mitaa, sehemu za umma, usafiri wa umma, kwenye magari, maeneo ya starehe, sehemu za mikusanyiko, klabu, hotelini, kwenye maduka au maeneo yoyote;

b) Anamtunza mtu anayeamini kuwa ana ugonjwa uliotangazwa kuwa unaambukizika atakaposababisha au kuruhusu mtu huyo kuweka watu wengine kwenye hatari ya kuupata ugonjwa huo kwa uwepo wake au mwenendo wake katika eneo lolote;

c) Anatoa, anaazimisha, anasafirisha nguo au matandiko yanayojulikana kuwa na ugonjwa uliotangazwa au unaoambukizika au kitu chochote ambacho anajua kimepata au kinaweza kubeba maambukizi hayo bila kuua vijidudu;

d) Anapanga, anaajiri au anaazimisha maeneo yoyote yenye maambukizi au ugonjwa uliotangazwa au mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo kabla ya kuua vijidudu;

Atakuwa ametenda kosa na anaweza kufungwa miezi 12 au kutozwa faini ya kiasi cha shillingi Millioni Moja au vyote viwili kwa pamoja.

Wito na Mapendekezo ya Mtandao:
• Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kutoa taarifa rasmi kwa umma juu ya maeneo yote yaliyotengwa ili umma kwa ujumla uyatambue maeneo hayo.

• Tunaendelea kuvihimiza vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuzingatia namna bora za ukamataji kama zilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Jeshi la Polisi na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Tunawapongeza askari polisi waliowakamata waandishi hao pamoja na mpiga picha kwa kutokutumia nguvu wakati wa kuwakamata.

• Tunaomba Jeshi la polisi, maofisa wa Afya na mamlaka nyingine husika kuweka matangazo hadharani kwenye maeneo yote yaliyozuiwa.

• Tunawashauri waandishi na wananchi kuepuka kwenda kwenye maeneo yaliyozuiwa na pale panapokuwa na haja ya kwenda maeneo hayo, basi watafute vibali vya kuingia maeneo hayo kutoka kwenye Wizara ya Afya.

• Tunaomba waandishi wanaodhamiria kutafuta taarifa kwenye maeneo ya karantini wapewe ruhusa na vifaa vya kujikinga ili kuepuka maambukizi.

• Ni muhimu kushirikisha Asasi za Kiraia katika kamati zinazoundwa kukabiliana na virusi vya korona kwa kuwa AZAKi ni wadau wakubwa katika kutatua changamoto za kijamii

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Machi 24, 2020.