TAMKO KUHUSU KUFUNGIWA NA KUPIGWA FAINI KWA VITUO VYA MTANDAONI VYA KWANZA TV, WATETEZI TV NA AYO TV

1.0) Utangulizi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unalaani vikali kitendo cha Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kufungia kituo cha Televisheni mtandaoni cha Kwanza TV, kwa muda wa miezi sita (6) pamoja na kupiga faini ya milioni tano (5,000,000) na onyo kwa televisheni nyingine mbili za mtandaoni, Ayo TV na Watetezi Tv.

2.0) Kuhusu Tuhuma na Adhabu Zilizotolewa

Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia ni kwamba, kituo cha Kwanza TV kimefungiwa kwa makosa mawili; Uchapishaji wa habari za upotoshaji mtandaoni zenye kichwa cha habari kisemacho “Gwajima apata ajali”, pamoja na kukiuka Kanuni ya 5 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018. Kanuni hiyo inamtaka kila mmiliki wa kituo cha mtandao kuchapisha Sera au Mwongozo wa watumiaji.

Vituo vya habari za mitandaoni vya Watetezi TV na Ayo TV vimepigwa faini ya fedha taslimu za kitanzania millioni tano (5,000,000) na kupewa onyo kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni ya 5 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018. Kanuni hiyo inamtaka kila mmiliki wa kituo cha mtandao kuchapisha Sera au Mwongozo wa watumiaji.

3.0) Uhalali wa Adhabu na Utaratibu Uliotumika

Kwa maelezo hayo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umesikitishwa na mchakato mzima wa namna ambavyo vyombo hivyo vimeitwa hadi kutolewa maamuzi. Kwani kituo cha Watetezi TV hakikupewa muda wa kutosha wa kujitetea mbele ya Kamati ya Maudhui. Watetezi Tv ilipokea wito wa kufika mbele ya Kamati majira ya sa 10:30 jioni siku ya jumatano tarehe 25/09/2019 na kutakiwa kufika mbele ya kamati siku ya Alihamisi tarehe 26/09/2019 mnamo majira ya 06: 00 mchana.

Aidha, pamoja na walalamikiwa wote kujieleza kwa ufasaha na kwa hoja zenye mashiko, bado kamati hiyo imeendelea kutoa adhabu haswa kwakuwa kanuni zenyewe zina utata ambao unaipa Kamati haki ya kutafsiri watakavyo. Walalamikiwa wote waliieleza Kamati kuwa wana Sera na Miongozo yao lakini Kanuni hazijasema bayana ni kwa namna gani wanatakiwa kuwapa wateja/walaji kwakuwa Mtandao wa YouTube una Kanuni na Masharti yake na kuwa kuweka Sera na Miongozo kwenye Mtandao huo kungesababisha TV zao kusitishiwa huduma. Hata hivyo, Kamati hiyo iliendelea kutoa adhabu hizo kwa kusisitiza kwamba, wamiliki wa TV hizo walitakiwa kuweka walau Sera na Miongozo ya kwa ufupi (Policy Statement) katika chaneli zao.

Mtandao umesikitishwa na adhabu zilizotolewa na Kamati kwakuwa kubwa na kutozingatia hali ya kiuchumi ya Televisheni hizo ukizingatia kwamba hazifanyi biashara bali kazi kubwa ni kuuhabarisha umma. Pia kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (2) cha Kanuni za Maudhui Mtandaoni, Kamati ilipaswa kuzipa TV hizo taarifa na kuzitaka kutekeleza vigezo na masharti ndani ya kipindi Fulani. Hata hivyo, kwa makusudi kabisa, Kamati iliamua kutoa adhabu ambayo kimsingi haiendani na makosa yanayodaiwa kutendwa.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unatoa wito kwa vyombo vya habari mtandaoni vilivyofungiwa na kuamriwa kulipa faini kuchukua hatua ya kukata rufaa kuhusu maamuzi yaliyotolewa na Kamati.

Ikumbukwe kwamba, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (THRC) pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT) walifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara kupinga Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), mwaka 2018. Kati ya hoja kuu za kufungua kesi hiyo ni utata wa kanuni hizo, Kanuni hizo kukiuka haki ya kupata na kusambaza taarifa kwa umma, kanuni zinakiuka haki ya watu kujieleza na adhabu yake ni kubwa ambayo haiendani na kosa. Kanuni hizo pia zinakiuka uhuru wa kujieleza na watu kutoa maoni yao sababu zinawalazimisha wamiliki wa vyombo vya mtandaoni kuchuja maoni ya watumiaji pamoja na kuweka masharti magumu ya usajili wa watoa huduma mitandaoni. Kesi hiyo kwasasa ipo katika ngazi ya rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kanda ya Mtwara.

Wakati maamuzi ya kesi hiyo hayajafikiwa, wala kanuni bado hazijakidhi matakwa ya haki za wamiliki wa vyombo vya mtandaoni na watumiaji wa mitandaoni tunaanza kuona madhara ya Kanuni hizi.

Hivyo basi, maamuzi ya Kamati ya Maudhui yaliyotolewa leo yanathibitisha mapungufu ya Kanuni hizo ambazo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania ulizibaini mapema na kufungua kesi mahakamani.

4.0 Wito wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

1) Vyombo vyote vilivyohukumiwa katika maamuzi ya Kamati ya Maudhui vitumie haki yao ya msingi ya kukata rufaa mbele ya Baraza la Ushindani wa Haki Kibiashara ndani ya siku 21 kuanzia leo ili haki ionekane kutendeka.

2) Mtandao unatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari mtandaoni, watumiaji wa mtandaoni, watunga sheria na wadau wote wa haki nchini kuendelea kupinga Kanuni hizi ambazo kimsingi zipo kinyume na misingi ya haki ya uhuru wa watu kujieleza kwa kutumia njia yoyote ile ambayo wao wameichagua ikiwemo kutumia mitandao.

Imetolewa leo tarehe 27/09/2019

Na:
Onesmo Olengurumwa,
Mratibu Kitaifa – THRDC