TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUNYIMWA DHAMANA WAANDISHI WA HABARI WATATU NA MMILIKI WA NJOMBE YETU TV

Njombe – Tanzania

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesikitishwa na kitendo cha kukamatwa na kunyimwa dhama kwa waandishi wa habari watatu wanaomiliki TV za Mtandaoni pamoja na mmiliki wa Njombe Yetu TV siku ya Jumamosi tarehe 29 Februari 2020. Waandishi hao ni: Prosper Daudi Mfugale mwandishi wa ITV ambaye anamiliki Njombe TV, Ibrahim Godfrey Mlele mwandishi wa TV E anamiliki Mlele TV, Dickson Khanyika mwandishi wa Star TV anamiliki Habari Digital TV, pamoja na Benedicto ambaye ni mmiliki wa Njombe Yetu TV.

Kuhusu Tuhuma na Kukamatwa kwao
Kwa mujibu wa taarifa toka kwa Wakili wa THRDC Mkoani Njombe ni kwamba, mnamo siku ya Jumamosi tarehe 29 Februari 2020, majira ya saa kumi jioni, waandishi wa habari wawili Prosper Daudi Mfugale, Ibrahim Godfrey Mlele na Benedicto walikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumiliki TV za Mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Pia, mwandishi Dickson Khanyika alikamatwa akiwa Morogoro mjini na kusafirishwa hadi kituo cha polisi Njombe mjini.

Kuhusu Dhamana yao
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kupitia wakili wake Chance Luoga, tumefatilia kupata dhamana ya waandishi waliokamatwa kwa siku mbili mfululizo. Dhamana imeshindikana kutolewa kwa siku zote mbili mfululizo kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi na Jeshi la Polisi mkoani Njombe. Hata hivyo Wakili Chance Luoga amepewa taarifa kuwa kesho Machi 4, 2020 waandishi hao wanaweza kufikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yao ikiwa ni siku ya 4 toka kukamatwa.

Wito wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

1) Jeshi la Polisi linapaswa kuzingatia haki za watuhumiwa hao ikiwemo kuwaachia huru au kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 [Toleo la mwaka 2002].

2) Ibara ya 13 ya Katiba inahitaji mtuhumiwa anapokuwa amekamatwa, kufikishwa mahakamani kwa haraka ili aweze kupata nafasi ya kujitetea/kujibu tuhuma zinazomkabili.

3) Mtandao unatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari mtandaoni, watumiaji wa mtandaoni, watunga sheria na wadau wote wa haki nchini kuendelea kupinga Kanuni hizi ambazo kimsingi zipo kinyume na misingi ya haki ya uhuru wa watu kujieleza kwa kutumia njia yoyote ile ambayo wao wameichagua ikiwemo kutumia mitandao. Ikumbukwe kuwa mitandao ya kijamii ipo bure kwa kila mtu duniani kutumia na wenye mitandao hii hawajawahi kudai wanaotumia walipie chochote.

 

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Machi 3, 2020