MWENYEKITI WA TUME YA UMOJA WA AFRIKA ALAANI VIKALI MAUAJI YA GEORGE FLOYD

MWENYEKITI WA TUME YA UMOJA WA AFRIKA ALAANI VIKALI MAUAJI YA GEORGE FLOYD

Addis Ababa, Ethiopia

Kufuatia mauaji ya kikatili ya raia wa kimarekani mwenye asili ya kiafrika, marehemu George Floyd (46) -aliyeuawa na polisi Derek Chauvin- huko jijini Minneapolis nchini Marekani mnamo tarehe 25 Mei 2020, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (African Union Commission) Mhe. Moussa Faki Mahamat amelaani vikali kitendo hicho kuwa cha kibaguzi, kikatili na cha kutweza utu wa binadamu.

Kupitia tamko lake lililochapishwa na Msemaji wa Ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Afrika siku 4 tu baada ya mauaji hayo kutokea, Mhe. Moussa Faki Mahamat amerejea ‘Azimio la kupinga ubaguzi wa rangi nchini Merikani la mwaka 1964‘.

Itakumbukwa kuwa, Azimio hili liliafikiwa na marais wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika walioshiriki mkutano mkuu wa kwanza wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Cairo, Misri kati ya tarehe 17 hadi tarehe 24 Julai 1964.

Kupitia mkutano huo, Azimio la kupinga ubaguzi wa rangi nchini Merikani la mwaka 1964 lilijumuisha makubaliano na msimamo wa marais wa nchi za Afrika dhidi ya ubaguzi wa wamarekani weusi wanaoishi Marekani.

Aidha, kupitia tamko hilo Mhe. Faki pia ametuma salamu za rambirambu kwa familia ya marehemu George Floyd na kuitaka Serikali ya Marekani kuweka jitihada za ziada kutokomeza kabisa ubaguzi wa rangi na hasa mauaji ya wamarekani weusi ambayo yameendelea kuwepo kwa zaidi ya karne moja sasa.

(Kusoma tamko hili kwa lugha ya kiingereza, tafadhali tembelea tovuti ya Tume ya Umoja wa Afrika: https://au.int/en/pressreleases/20200529/statement-chairperson-following-murder-george-floyd-usa)

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

Leo tarehe 31 Mei, 2020