MWANDISHI ERICK KABENDERA AHUKUMIWA KULIPA FAINI YA ZAIDI YA MILIONI 200

Dar es Salaam – Tanzania

Hatma ya Mwandishi wa Habari za kiuchunguzi Ndugu Erick Kabendera imefikia tamati leo tarehe 24 Februari 2020 baada ya kusaini mkataba wa makubaliano ya kukiri kosa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (Director of Public Prosecutions – DPP). Ikumbukwe kuwa, mwandishi Erick Kabendera alikamatwa mnamo tarehe 29 Julai 2019 na tangu kukamatwa kwake alifikishwa mahakamani mara 19 bila upelelezi kukamilika.

Katika hukumu ya kesi yake, leo upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Reginald Martin pamoja Wakili Jebra Kambole, pia THRDC iliwakilishwa na Mwanasheria Paul Kisabo aliyehudhuria mahakamani hapo kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kesi hiyo. Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wawili, Wakili Faraja Nchimbi na Wakili Wankyo Simon.

Wakili Faraja Nchimbi alianza kwa kuiambia mahakama kwamba, mshitakiwa Erick Kabendera yupo mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ameridhia maombi ya kukiri kosa yaliyowasilishwa na mshitakiwa kwa mujibu wa kifungu namba 26(1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200. Wakili Nchimbi pia alisema kuwa, DPP aliipa hati mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza shauri hilo la Uhujumu Uchumi kwa mujibu wa kifungu namba 12(3)& (4) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200.

Wakili Nchimbi alisema pia kuwa, DPP alithibitisha kuridhia kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa (Plea Agreement) na mshitakiwa Erick Kabendera kwa mujibu wa kifungu namba 194 C (3). Pia Wakili Nchimbi aliwasilisha nakala za makubaliano (Plea Agreement) mbele ya mahakama ambayo ilikwishasainiwa na Wakili Nchimbi kwa niaba ya DPP, mshitakiwa Erick Kabendera, dada yake Prisca Kabendera pamoja na wakili wake Wakili Jebra Kambole.

Baada ya kuwasilisha nakala hizo Mhe. Hakimu Janeth Mtega alisema kuwa, “…Kwa mujibu wa kifungu namba 198(A) (1)&(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20, nimepokea nakala hizo…”

Wakili Nchimbi aliendelea kusema kuwa, kwa mujibu wa sehemu (B) aya ya 6 ya Mkataba wa Makubaliano (Plea Agreement), DPP aliridhia kuondoa kosa la kwanza la Kuongoza Genge la Uhalifu.

“…Kwa mujibu wa kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20, naomba kuifahamisha mahakama kwamba tumeondoa shitaka la kwanza na hivyo kubakiwa na shitaka la pili na la tatu”, aliongeza Wakili Nchimbi.

Baada ya hapo, Erick Kabendera aliapishwa kwa mujibu wa kifungu namba 194 (E) (i) cha Sheria ya Mwenedo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 na kuelezwa matokeo ya kiapo chake juu ya kukiri kosa kuwa hawezi kukata rufaa juu ya kile ulichokiri isipokuwa anaweza kukata rufaa juu ya hukumu yake.

Wakili Nchimbi pia alisema, kwa mujibu wa kifungu namba 194 (D) (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20, mtuhumiwa anapaswa kuonesha wazi utayari wake wa kukiri kosa ili mahakama iweze kutunza kumbukumbu hiyo. Hivyo, Mhe. Hakimu Janeth Mtega alimuuliza mshitakiwa Erick Kabendera kama alifanya makubaliano hayo bila kulazimishwa. Erick Kabendera alikiri mbele ya mahakama kuwa hakulazimishwa na mtu yeyote kukiri makosa.

Baada ya hapo, Wakili wa upande wa Jamhuri Wakili Wankyo Simon alimsomea Erick Kabendera mashitaka mawili yaliyobaki ambayo ni: Kushindwa kulipa kodi kiasi cha fedha taslimu za kitanzania 173, 247,470/= kinyume na kifungu namba 105 (a) cha Sheria ya Kodi. Na kosa la pili ni Kutakatisha Fedha taslimu za kitanzania millioni 173 kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi. Mwandishi Erick Kabendera, alikiri makosa yake yote mawili.

Wakili Nchimbi alisema pia kwamba, kwa mujibu wa kifungu namba 194 (1)(a)&(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mtuhumiwa anapaswa kusomewa masharti ya makubaliano yake na DPP. Wakili Wankyo Simon alimsomea mshitakiwa masharti hayo ambayo yanajumuisha makosa yake mawili aliyokiri pamoja na ridhaa ya DPP juu ya maombi ya kukiri kosa.

Baadhi ya masharti ya Mkataba wa Makubaliano na DPP ni kwamba endapo Erick Kabendera atakiuka masharti ya makubaliano hayo, DPP atakuwa na mamlaka ya kumfungulia upya Erick Kabendera mashitaka hayo ambayo yameondolewa wakati wa makubaliano ya kukiri kosa.

Masharti mengine ni kwamba, Erick Kabendera atatakiwa kulipa faini kadiri ya makubaliano ndani ya miezi 6 kwa awamu sita kila tarehe 30 ya mwisho wa mwezi. Pia, atashirikiana na DPP kutoa taarifa zote za makosa yake. Wakili wa Erick Kabendera hakuwa na pingamizi lolote juu ya kilichowasilishwa mahakamani.

Mhe. Hakim Janeth Mtega kabla ya kutoa hukumu, alimwomba wakili wa Serikali kutoa historia ya makosa ya mshitakiwa. Wakili Nchimbi alisema kwamba Mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo akaiomba mahakama katika kutoa hukumu ijielekeze Sehemu (B) aya ya 7 na 8 ya Mkataba wa Makubaliano wa Kukiri Kosa.

Wakili wa upande wa utetezi Wakili Jebra Kambole naye aliisihi mahakama kabla ya kutoa hukumu, izingatie kuwa hii ni mara ya kwanza Erick Kabendera kushitakiwa. “Tangu tarehe 5 Agosti 2019, mshitakiwa alikuwa magereza na amekuwa akifika mahakamani. Ana familia inayomtegemea na pia afya yake sio njema. Tunaomba mahakama impatie adhabu ndogo na naiomba mahakama ijikite sehemu (B) aya ya 8 ya Makataba wa Makubaliano ya Kukiri Kosa.”, alisema Wakili Jebra Kambole.

Baada ya mawasilisho yote, Hakimu Janeth Mtega kwa mamlaka aliyopewa, alimtia hatiani Erick Kabendera kwa makosa yote mawili aliyokiri.

Kwa kosa la kwanza, Hakimu Janeth Mtega amemuhukumu Erick Kabendera kulipa shilingi laki mbili na elfu hamsini (TZS 250,000/=) pamoja na fidia ya shilingi 172,247,047/= za kitanzania.

Kwa kosa la pili, Hakimu Janeth Mtega amemuhukumu Erick Kabendera kulipa kiasi cha shilingi milioni mia moja za kitanzania (TZS 100,000,000/=).

 

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Leo tarehe 24 Februari 2020