MWANAHARAKATI NCHINI TANZANIA KUPINGA WATUHUMIWA KUSHTAKIWA KWENYE MAHAKAMA ZISIZOKUWA NA MAMLAKA YA KUSIKILIZA KESI ZAO (COMMITAL PROCEEDINGS)

Dar es Salaam – Tanzania

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa amefungua kesi namba 36 ya mwaka 2019 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam akipinga watuhumiwa wa makosa mbalimbali nchini humo kufikishwa kwenye mahakama zisizokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi zao (Committal Proceedings).

Katika kesi hiyo, mwanaharakati huyo wa haki za binadamu nchini Tanzania, anapinga ukamatwaji wa watuhumiwa wa makosa mbalimbali bila upelelezi kukamilika.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa leo tarehe 13 Februari 2020 kwa mara ya kwanza majira ya saa saba mchana mbele ya majaji watatu, Jaji Masoud, Jaji Mlyambina na Jaji Juliana Masabo.

Akizungumzia msingi wa kesi hiyo aliyoifungua tangu Desemba 16, 2019, Olengurumwa amesema kuwa analenga kuiomba Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa tamko la kufuta vifungu vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (Toleo la mwaka 2002), ambavyo amedai vinakiuka haki na uhuru wa watuhumiwa, kuminya utawala wa sheria, na kufifisha mchakato mzima wa uendeshaji wa kesi kwa usawa, sababu ambayo ameitaja kuwa inahamasisha matumizi mabaya ya mamlaka ikiwemo kufanya upelelezi kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Olengurumwa amesema kesi hiyo pia inalenga kuiomba mahakama hiyo kutoa tamko kwamba kifungu namba 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, 258 na 259 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (Toleo la mwaka 2002) kuwa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 na kwamba vifungu hivyo vinapaswa kufutwa na kuondolewa kabisa.

Olengurumwa ambaye ni msomi wa sheria na mchambuzi wa sera za umma nchini Tanzania ameeleza zaidi kuwa mtuhumiwa anapofunguliwa mashtaka kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi yake, mtuhumiwa huwa haruhusiwi kusema chochote, hivyo humfanya akose haki yake ya msingi ya kusikilizwa kwa wakati.

Akifafanua zaidi amesema kuwa sheria nayo pia bado haijaweka utaratibu wa namna ya kuhakikisha upelelezi unafanyika haraka na kwa wakati ili kuhakikisha kwamba mtuhumiwa anafikishwa mbele ya mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi yake.

Akinukuu kifungu namba 178 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (Toleo la mwaka 2002), Olengurumwa amesema kifungu hicho kinasema, “Pale ambapo kesi itafunguliwa kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kuisikiliza, baada ya upelelezi kukamilika, mahakama hiyo inapaswa kutoa amri ya kesi hiyo kwenda kusikilizwa mahakama kuu.”

Olengurumwa ameelezea changamoto ya kifungu hicho ambapo amedai kuwa, kwakuwa upelelezi umekuwa ukichukua muda mrefu kwenye kesi nyingi ama pengine kutokamilika, kifungu hiko cha 178 kimekuwa hakina uhalisia, hivyo kinastahili kufutwa.

Olengurumwa ameeleza kuwa Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaweka bayana kuwa, Bunge linawajibu wa kutunga sheria ambazo hazikinzani na Katiba.

Vilevile, Olengurumwa ameeleza zaidi kuwa, serikali ina wajibu wa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.