MWANAHARAKATI NA MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TITO MAGOTI AKAMATWA NA WATU WASIOJULIKANA

Dar es Salaam – Tanzania

Taarifa zilizotufikia hivi punde ni kwamba, Mtetezi wa Haki za binadamu ambaye pia ni Afisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) amekamatwa asubuhi ya leo na watu watano akiwa kwenye kituo kimoja cha mafuta maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam na kisha kutokomea naye kusikojulikana.

Watu hao ambao walitumia nguvu kumuingiza Tito kwenye gari aina ya Harrier walikuwa wamevaa kiraia. Jitihada za kumtafuta ndugu Tito Magoti katika vituo mbalimbali vya polisi zinaendelea.

Sisi kama Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) tumesikitishwa sana na tukio hili kwani matukio kama haya ya utekwaji nchini yameendelea kushamiri hasa dhidi kwa Watetezi wa Haki za Binadamu.

Tunaliomba jeshi la polisi kuchukua hatua za haraka na za maksudi kuhakikisha mtetezi Tito Magoti anapitakana akiwa salama.

Tunawaomba pia watetezi wote wa haki za binadamu nchini, wanahabari na wadau wengine wa haki za binadamu, tuungane kupaza sauti zetu kwa ajili ya Mtetezi mwenzetu.

THRDC itaendelea kuwapa taarifa zaidi juu ya hili kadri tutakavyokuwa tunazipata.

#BringBackAliveTitoMagoti

#BringBackAliveTitoMagoti

#BringBackAliveTitoMagoti

Imetolewa na: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Leo tarehe 20.12.2019