Mratibu Kitaifa THRDC, Onesmo Olengurumwa akiongozana na Afisa dawati la wanachama, Bi Lisa Kagaruki, wametembelea taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa upande wa Tarime mkoa wa Mara.
CDF inayojihusisha na maswala ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambapo ofisi kuu ipo Daresalaam kanda ya Pwani, na moja matawi yake ipo mkoa wa Mara.

Taasisi hii imekuwa ikifanya kazi na jamii kwa ukaribu hasa katika kuibua vitendo vya kikatili vinavyowakumba watoto pamoja na wanawake.
Kwa mkoa wa Mara, CDF inaendesha programu tatu ambazo ni Ulinzi wa Mtoto, Uwezeshaji msichana kiuchumi, na Program ya Ushirikishwaji. Programu zote tatu zikilenga ujenzi wa jamii inayojali utu wa mtoto.

CDF Mara inajivunia kusukuma gurudumu la kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa kupitia wanaume wa jamii ya Mkoa wa Mara. Programu ya ushirikishwaji imeweza kuwajengea uwezo wababa kuhusu umuhimu wa kusimamia haki ya mtoto na mwanamke. Hii hufanyika kupitia vikundi vya wababa vilivyoundwa na kuratibiwa na shirika. Kuna jumla ya vikundi 5, ambapo kikundi kimoja kina wababa 15 kutoka kila kata.

Shirika hili hufanya uchechemuzi na kuibua masuala mbalimbali ya ukatili na mila kandamizi katika jamii.
CDF imekumbana na changamoto kadha katika utekelezaji wa kazi za kitetezi ambazo ni pamoja na;
Pale taasisi inapofanya kazi na viongozi wa kimila na kidini katika kutokomeza ukatili kwa makundi tajwa bado utekelezaji unakuwa mgumu kwani viongozi hao wamefungwa na mila na desturi zao.
Kuwepo kwa uelewa mdogo wa maswala yahusuyo kazi za utetezi wa haki za binadamu unaleta changamoto kubwa katika ngazi za maamuzi, kesi nyingi hazifiki maamuzi ya kisheria.
Changamoto za kiusalama, ambapo watendaji wamekiri kupata vitisho kutoka kwa jamii. Pia Mabalozi wa CDF wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa wazee wa kimila juu ya mafunzo yanayotolewa na taasisi hii juu ya kuondokana na mila potofu zinazoikandamiza jamii yetu hasa ukeketaji, na mimba za utotoni. Changamoto nyingine ni pamoja na utayari wa serikali kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya masuala ya haki za watoto kwa wilaya ya Tarime.

Pamoja na changamoto hizo taasisi bado inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa haki za binadamu kuanzia ngazi za familia, viongozi wa serikali, viongozi wa dini na baadhi ya viongozi wa kimila hii imesaidia kupungua kwa baadhi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto.

Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa ameipongeza sana CDF kwa maendeleo makubwa. Pia ameishauri CDF kuwahamasisha wanachama wa mtandao kushiriki katika michakato mbali mbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa juu ya utetezi wa haki za mtoto. Pia amehamasisha shirika kuendelea kushirikiana na Mtandao.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
12 Agosti 2021