MRATIBU THRDC AKUTANA NA BAKWATA

Dar es Salaam, Tanzania

Leo Juni 28 2021, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii – BAKWATA, Bi. Asina Shunduli ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa BAKWATA, amekutana na Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa kwa ajili ya maongezi mafupi.

Katika mazungumzo na Bi. Shunduli, Mratibu Kitaifa wa THRDC Wakili Olengurumwa amepata fursa ya kuikaribisha rasmi BAKWATA kama moja ya Taasisi za Kidini, yenye Asasi za Kiraia zinazotoa Huduma kwa Jamii katika Maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini Tanzania maarufu kama ‘Defenders Day’ yanayotarajiwa kufanyika Julai 2, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Maadhimisho haya yatahudhuriwa na Watetezi wa Haki za Binadamu, Viongozi wa Serikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali Pamoja na Taasisi mbali mbali za Kidini.

Wakili Olengurumwa pia amepata alimwelezea Bi. Shunduli Dhima Kuu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Kujadili Mchango wa Asasi za Kiraia katika Utekelezaji Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano ya Maendeleo ya Taifa”. Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

Aidha, Baraza Kuu la Waisilam Tanzania (BAKWATA) limethibitisha Ushiriki wa karibu katika maadhimisho hayo ambapo litawakilishwa na Katibu Mkuu wa Baraza hilo.

Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Leo Juni 28, 2021